Wabunge wapya waapishwa Msumbiji
13 Januari 2025Wakati wa kuapishwa kwa bunge jipya la Msumbiji mapema leo, vyama vidogo viwili va upinzani vilisusia hafla ya ufunguzi wa bunge. Vyama hivyo vimechukua hatua hiyo kwa madai kuwa havikukubali matokeo ya uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba. Hayo yamejiri wakati Rais anayeingia madarakani Daniel Chapo akitoa wito wa kudumisha hali ya utulivu na umoja baada ya miezi kadhaa ya machafuko.
Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane, ambaye ni maarufu miongoni mwa vijana anadai kuwa matokeo ya uchaguzi yaligubikwa na udanganyifu na kukipa ushindi chama cha Frelimo ambacho kimekuwa madarakani kwa miaka 50.
Soma zaidi: Kiongozi wa upinzani Msumbiji aitisha maandamano kwa siku tatu
Mwishoni mwa juma, Mondlane aliwataka wafuasi wake kuonesha kwa vitendo kuwa wanayakataa matokeo rasmi ya uchaguzi kuanzia Jumatatu hadi Jumatano wakati Rais Mteule atakapoapishwa kama Rais wa Msumbiji.
Katika shughuli ya kuapishwa kwa wabunge, jeshi lililizunguka jengo la bunge na polisi walifunga barabara kuu kadhaa zinazoingia katika eneo hilo. Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa katikati ya mji ambako huwa na shughuli nyingi Jumatatu hasa palionekana patupu na maduka mengi yalifungwa lakini kwenye baadhi ya maeneo waandamanaji waliweka vizuizi.
Rais mteule Chapo na Filipe Nyusi washiriki kuapishwa kwa wabunge
Chapo na Rais anayemaliza muda wake Filipe Nyusi walihudhuria hafla hiyo wakati wabunge wa chama chao cha Frelimo kilichoshinda viti 171, na chama cha Podemos kilichopata viti 43 walipoapiishwa. Wabunge 28 wa chama cha Renamo na wengine 8 wa MDM walisusia shughuli hiyo. Mondlane, kupitia ukurasa wake wa Facebook alisema siku ya Jumamosi kuwa, kama bunge hilo lingeapishwa kitendo hicho kingekuwa usaliti wa matakwa ya wananchi.
Kulingana na matokeo rasmi Rais mteule Daniel Chapo alipata asilimia 65 ya kura wakati Mondlane alipata asilimia 24 pekee. Hata hivyo Mondlane anadai kuwa allishinda uchaguzi huo kwa asilimia 53 na taasisi za uchaguzi za Msumbiji ziliyachakachua matokeo. Alirejea nyumbani Alhamisi akitokea mafichoni baada ya mwanasheria wake kuuwawa kwa kupigwa risasi.
Maelfu ya wafuasi wake walikusanyika kumpokea, hali iliyoibua mapigano kati yao na wanausalama. Hadi sasa, ghasia zilizotokana na uchaguzi wa Oktoba 9, zimeshasababisha jumla ya karibu vifo vya watu 300 wakiwemo polisi, kulingana na shirika la ndani la haki za binadamu. Jeshi la polisi nchini humo, linalaumiwa kwa kutumia nguvu kubwa ikiwemo matumizi ya risasi dhidi ya waandamanaji.