Seneti ya Marekani yachukua hatua ya kihistoria.
24 Desemba 2009Wananchi wa Marekani zaidi ya milioni 30 ambao hadi sasa hawakuwa na bima ya afya, leo tayari wamepata zawadi ya krismasi baada ya Seneti ya nchi hiyo kuupitisha mswada juu ya kuleta mageuzi makubwa katika mfumo wa afya.
Baada ya kuruka kiunzi cha Baraza la Wawakilishi, mpango wa rais Barack Obama juu ya kuleta mageuzi katika mfumo wa afya leo umepitishwa na Baraza la Seneti.
Maseneta 58 wa chama cha Demokratik na wawili wasiokuwa na chama chochote waliupitisha mswada wa kuleta mageuzi hayo.Lakini maseneta 39 wa chama cha Republican waliupinga.
Lengo la mageuzi hayo ni kuwapa wamarekani milioni 30 bima ya afya. Mswada huo pia utazikataza kampuni za bima kuwanyima watu huduma ati kwa sababu ya hali zao za afya za tokea zamani.
Hatahivyo mswada huo bado utahitaji uoanishwe na mswada mwingine wa Baraza la Wawakilishi ili uweze kutiwa saini na rais Obama.
Maseneta wote wa chama cha Republican waliupinga mswada huo wa mageuzi ya afya.
Mageuzi ya mfumo wa afya ni suala la kipaumbele katika sera za ndani za rais Obama. Kupitishwa mswada huo leo na maseneta kutawapa mamilioni ya wamarekani haki ya kupata huduma za afya zenye uhakika.
Rais Obama amesema kupitishwa kwa mswada huo leo ni hatua ya kihistoria . Rais huyo amesema , sasa Marekani inakaribia kufikia lengo la kutekeleza ahadi ya kuleta mageuzi madhubuti katika bima ya afya.Obama amesema sasa Marekani ipo karibu sana na kuyafanya mageuzi ya bima ya afya kuwa hali halisi nchini Marekani.
Mwandishi / Mtullya Abdu.
Mhariri/ Saumu Yusuf