1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUfaransa

Mswada wa sheria ya uhamiaji wa Ufaransa wasababisha ghasia

11 Desemba 2023

Rais Emmanuel Macron anataka kufanyia mageuzi sheria ya uhamiaji na hatua za kuwahamisha kutoka nchini humo, lakini wahamiaji na wakimbizi wanaopinga mageuzi hayo wamesema ukali wa hatua hizo mpya haujawahi kushuhudiwa

Picha iliyotolewa na Walinzi wa Pwani ya Ugiriki ikionyesha meli ikiwa na idadi kubwa ya wahamiaji  kusini-magharibi mwa Peloponnese, Jumatano, Juni 14, 2023.
Picha ya walinzi wa Pwani ya Ugiriki ikionesha meli ikiwa na idadi kubwa ya wahamiaji Kusini-magharibi mwa PeloponnesePicha: Griechische Küstenwache/Eurokinissi/ANE/picture alliance

Maelfu ya watu waliandamana katika barabara karibu na kituo cha treni cha Montparnasse Kusini mwa Paris katika Jumapili moja ya hivi karibuni. Waandamanaji hao walikuwa wameshikilia mabango ya kutangaza upinzani wao kwa "sheria ya Darmanin," iliyopewa jina la waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Gerald Darmanin. Mabango mengine yalikuwa na ujumbe uliosema "Uhamiaji sio tatizo, tatizo ni ubaguzi wa rangi.

Soma pia: Macron asifu makubaliano ya kutatua mkwamo wa uhamiaji Ulaya

Aliyekuwa mstari wa mbele katika maandamano hayo na simu kubwa mkononi ni Ahmada Siby. Mwanamume huyo kutoka Mali wa umri wa miaka 33, aliwasili Ufaransa takriban miaka mitano iliyopita. Akinufaika kutokana na mwanya wa kisheria, amekuwa akitumia karatasi za watu wengine kufanya kazi ya kusafisha, ujakazi na hivi karibuni, kuosha vyombo.

'Tunafanya kazi zote chafu'

"Wengi wetu wahamiaji wasio na vibali tunatumia njia hii, lakini ina maana kwamba tunalipa ada za bima ya kijamii na kodi bila kufaidika na huduma kama vile huduma za afya za umma kama raia wa Ufaransa," ameiambia DW.

Hii ndio maana Siby na wengine wameungana kupinga mswada huo, ambao serikali ya Ufaransa imesema ni maafikiano yanayojumuisha hatua za mrengo wa kushoto na kulia.

Uhamishaji ni rahisi, kuunganisha familia ni ngumu zaidi

Rasimu hiyo ya sheria inatazamiwa kujadiliwa katika bunge la Ufaransa, kuanzia Desemba 11, na inaweza kuanza kutumika mapema mwaka ujao.

Toleo la mwisho la mswada huo wa uhamiaji bado linahitaji kufanyiwa maamuzi, lakini baadhi ya maelezo tayari yanajulikana.

Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Ludovic Marin/AP Photo/picture alliance

Mswada huo mpya huenda ukaharakisha taratibu za kupata hifadhi na kufupisha muda wa kusikizwa kwa rufaa, kufanya kuungana tena kwa familia kuwa vigumu zaidi na kuzuia uwezekano wa kusafiri hadi nchini humo kwa matibabu.

Soma pia:Paris yaanza kuwaondoa wahamiaji

Mabadiliko pia yanajumuisha chaguo la kuwahamisha kutoka nchini humo watu ambao walikuwa na umri wa chini ya miaka 13 walipokuja Ufaransa, na pia kuwafukuza wazazi wa kigeni ambao watoto wao wana uraia wa Ufaransa.

Ufaransa ilikuwa inapanga kuanzisha kadi ya kijani ya mwaka mmoja kwa watu wanaofanya kazi katika sekta zilizo na uhaba wa wafanyikazi. Lakini kwa hali ilivyo sasa, maamuzi ya vibali hivi vya mwaka mmoja yameachiwa mamlaka za mitaa.

Ufaransa 'yapitisha kiwango kipya cha ukakamavu'

Lise Faron kutoka shirika lisilo la kiserikali la Cimade lenye makao yake mjini Paris linalotoa msaada kwa wakimbizi na wahamiaji, ni miongoni mwa wale ambao wana wasiwasi mkubwa kuhusu mswada huo mpya.

Faron ameiambia DW kwamba serikali ilikuwa imeahidi mswada wa uwiano, ilhali, sheria hizo mpya zinakaribia kuzuia kabisa haki za wahamiaji na kuifanya iwe vigumu zaidi kwao kuhalalishwa, hali itakayosababisha wahamiaji wengi zaidi wasio na vibali.

Soma pia:Wahamiaji vijana waunda kambi ya maandamano Paris

Faron ameongeza kuwa Ufaransa imepigia kura miswada mingi ya uhamiaji, lakini anahisi kama inapitisha kiwango kipya cha sheria kali kupitia mswada huo, kwa mfano kwa kurahisisha kuwafukuza wazazi wa kigeni wa watoto wenye uraia wa Ufaransa, ambayo iliwezekana hapo awali ikiwa walifanya uhalifu mkubwa.

Je, sheria mpya za uhamiaji zitakuwa na athari?

Alexis Izard, mbunge wa Essonne Kusini mwa Paris, amesema mswada wa mwisho bado utakuwa na uwiano.

Ameiambia DW kwamba kila mwaka wanahitaji kuwafurusha takriban wahamiaji haramu 4,000 ambao wamefanya uhalifu na hilo litawezekana kupitia sheria hiyo mpya, akiongeza kwamba hatua za kuwahamisha wahamiaji hao kutoka nchini humo zitachukuwa mwaka mmoja badala ya miwili baada ya marekebisho hayo.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW