1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtambo wa nishati ya nyuklia washambuliwa Ukraine

Sylvia Mwehozi
4 Machi 2022

Kituo cha mtambo mkubwa wa nishati ya nyuklia barani Ulaya kilichoko Ukraine kimelengwa katika mashambulizi ya Urusi usiku wa kuamkia leo Ijumaa wakati Urusi na Ukraine zikikubaliana kutenga njia salama kuhamisha raia.

Ukraine Kernkraftwerk Saporischschja
Picha: Photoshot/picture alliance

Waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ametaka kusitishwa mara moja kwa mapigano katika eneo hilo ili kuepusha maafa. Msemaji wa mtambo huo wa Zaporizhia Andrei Tuz, amesema shambulio la makombora lililofanywa na vikosi vya Urusi, limesababisha moto kuwaka katika mojawapo ya sehemu ya kituo hicho.

Ameongeza kuwa vikosi vya Urusi vinafyatua risasi kutokea pande zote kuelekea mtambo huo. Hapo awali shirika la kimataifa la udhibiti wa matumizi ya nyuklia IAEA lilikuwa limetoa tahadhari baada ya wanajeshi wa Urusi kuingia katika mji wa karibu wa Enerhodar kusini mwa Ukraine. Urusi imezidisha mashambulizi yake huku kukiwa na ripoti za vifo vya raia na uharibifu mkubwa. 

Hali ilivyo kwa wanafunzi wa Afrika Mashariki Ukraine

This browser does not support the audio element.

Mazungumzo ya Urusi na Ukraine

Wakati huo Urusi na Ukraine zimekubaliana juu ya hitaji la kutenga njia salama ya kupitisha misaada ya kiutu na uwezekano wa kusitisha mapigano kwa raia wanaokimbia machafuko. Pande zote mbili zimedokeza juu ya hilo baada ya mazungumzo ya jana Alhamis, ambayo ni ishara ya kwanza kuelekea uwezekano wa kupatikana mwafaka tangu kuanza kwa uvamizi.

Lakini  wakati mzungumzaji mkuu wa Urusi katika majadiliano hayo Vladmir Medinsky akisema kuwa mazungumzo yao yamekuwa na "maendeleo makubwa" vikosi vya Urusi vimeizingira na kuishambulia miji ya Ukraine wakati mzozo huo ukiingia wiki yake ya pili.

Kwa upande wake mjumbe wa Ukraine amesema mazungumzo hayo hayajazaa matunda ambayo Kyiv ilikuwa ikiyatarajia, lakini pande zote mbili zimekubaliana juu ya suala la kuwahamisha raia. Mshauri wa rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak amesema wanatarajia uwezekano wa usitishaji mapigano kwa muda ili kuruhusu uhamishaji wa raia na uundaji wa njia salama ya kibinadamu.

"Hii ni kusema kwamba sio kila mahala, lakini ni katika yale maeneo ambayo njia hizo salama za kiutu zitakuwa zimeainishwa, itawezekana kusitisha mapigano kwa kipindi chote cha kuwahamisha watu".

Rais Vladimir Putin na Rais Volodymyr ZelenskyyPicha: Russia/Ukraine Press Offices/AP/picture alliance

Pia wajumbe hao wamekubaliana juu ya usambazaji wa madawa na vyakula katika maeneo ambako mapigano makali yanaendelea. Wawakilishi katika mazungumzo hayo watakutana tena wiki ijayo, hayo ni kulingana na shirika la habari la Belarus Belta.

Putin na Zelenskiy watoa hotuba

Mjini Moscow kwenyewe, rais Vladmir Putin akipuuzia juu ya mito mbalimbali ulimwenguni ya kulaani uvamizi wake, amesema oparesheni za kijeshi zinaendelea kama zilivyopangwa na amewasifu askari wa nchi hiyo kuwa ni mashujaa wakati wa hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya Televisheni.

Awali rais Volodymyr Zelenskiy wa Ukraine alisema Kyiv na Moscow bado zinaweza kutafuta njia ya kumaliza vita hiyo ikiwa Kremlin itaichukulia Ukraine kwa usawa na kuingia katika mazungumzo kwa nia njema

"Kuna mambo ambayo yanaweza kupatikana mwafaka ili watu wasiendelee kufa, lakini kuna mambo ambayo hatuwezi kuyakubali", alisema Zelenskiy wakati wa mahojiano yake kwa njia ya Televisheni na akaongeza kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Putin.

Kwa upande mwingine mzozo wa kibinadamu umezidi kuwa mbaya huku Marekani ikisema watu karibu milioni moja wamekimbia makaazi yao hadi kufikia sasa. Wengi wao wanatafuta hifadhi nchini Poland na nchi nyingine za jirani.

Kifaru cha UrusiPicha: Russian Defense Ministry/AP Photo/picture alliance

Askari wa Ukraine pamoja na raia wameendeleza upinzani dhidi ya mashambulizi ya Urusi. Vikosi vya Urusi vilikuwa vikipambana kuudhibiti mji muhimu wa uzalishaji mafuta ulioko kusini mwa Ukraine. Mji huo wa Enerhodar ulioko katika mto Dnieper ndio unazalisha karibia robo ya umeme kote nchini Ukraine. Meya wa mji huo amesema askari wa Ukraine wanapambana vikali na wanajeshi wa Urusi.

Mapigano makali yameripotiwa nje kidogo ya mji wa kimkakati wa bandari wa Mariupol katika bahari ya Azov. Mashambulizi ya mabomu pia yamesikika kwenye mji mwingine wa kaskazini wa Chernihiv ambako maafisa wa huduma ya dharura wamethibitisha watu 33 kuuwawa na wengine 18 kujeruhiwa.

Kulingana na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa takribani watu 227 wameuawa na 525 kujeruhiwa. Urusi kwa upande wake imekiri kuwa askari wake wapatao 500 wamepoteza maisha tangu uvamizi huo ulipoanza, ingawa Ukraine inadai kuwa imewaua askari 9,000 wa Urusi, taarifa ambazo hazijathibitishwa.

Belarus, Eritrea, Syria na Korea Kaskazini ni mataifa yaliyopinga azimio la dharura la kupinga uvamizi wa Urusi nchini Ukraine katika Mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW