1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtandao wa Facebook wazimwa Myanmar

4 Februari 2021

Majenerali wa Myanmar wameamuru watoa huduma za mtandao kuuzuwia Facebook, baada ya katibu mkuu wa Umoja Mataifa Antonio Guterres kusema ulimwengu lazima ujipange ili kuhakikisha mapinduzi ya kijeshi yanashindwa.

	
Weltspiegel 04.02.2021 | Myanmar, Protest nach Putsch
Picha: REUTERS

Taifa hilo la Kusini mashariki mwa Asia limerudi katika utawala wa moja kwa moja wa kijeshi siku ya Jumatatu wakati Aung San Suu Kyi na viongozi wengine wa kiraia walipokamatwa katika msururu wa uvamizi wa alfajiri na kukomesha demokrasia iliyodumu katika taifa hilo kwa muda mfupi tu.

Wanajeshi wamekuwa wakishika doria katika mitaa ya miji mikubwa, na kufikia sasa hatua ya jeshi kutawala eneo hilo bado haujaibua maandamano makubwa ya kuunga mkono demokrasia. Badala yake watu wametumia mtandao wa kijamii wa Facebook kupaza sauti ya kupinga hatua ya jeshi na kuhamasisha maandamano ya kiraia.

Mwanajeshi wa MyanmarPicha: Stringer/AA/picture alliance

Kuzuia mtandao ni kubana uhuru wa vijana

Telenor, mmoja wa watoa huduma wakuu wa simu Myanmar wamethibitisha kwamba mamlaka imewamuru "kuzuia kwa muda" upatikanaji wa Facebook. NetBlocks, kampuni inayofuatilia kukatika kwa mtandao ulimwenguni kote, imesema kuzimwa kwa mtandao Myanmar kumeathiri programu zinazomilikiwa na Facebook kama vile Instagram na WhatsApp.

"Kuzuia Facebook leo inamaanisha kuwa uhuru wa vijana umezuiliwa kuanzia sasa. Mimi ni mwanafunzi. Elimu yetu imesimamishwa na biashara kukwama wakati mzozo wa janga la corona unaoendelea. Mapinduzi haya ya kijeshi yameanza kutupotezea kazi na elimu yetu sasa ipo kwenye matatizo." amesema mmoja wa watumiaji wa mtandao wa kijamii wa Facebook ambaye pia ni mwanafunzi wa chuo kikuu na mtafanyakazi wa teknolojia.

Aung San Suu kyi Picha: Thet Aung/AFP/Getty Images

Mashtaka Aung San Suu Kyi

Kwa mujibu wa msemaji wa chama cha Umoja wa Kitaifa kwa Demokrasia (NLD), Kyi Toe, Mahakama ya Myanmar hapo jana imemfungulia mashtaka Aung San Suu Kyi, kwa tuhuma za ukiukaji sheria kuhusu uagizaji na uuzaji bidhaa kimataifa.

Marekani na Uingereza zimelaani mashtaka hayo na kutaka aachiliwe mara moja.

Mkuu wa jeshi Min Aung Hlaing ameiacha jamii ya kimataifa ikihangaika kutafuta majibu, Na Katibu mkuu wa Umoja Mataifa Antonio Gutteres amesema atawashawishi majerali wa Myanmar kusitisha mapinduzi .

Waziri wa Mambo ya nje wa Uingereza Dominic Raab kupitia mtandao wake wa twitter amelaani mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya kiongozi aliyepinduliwa Myanmar Aung San Suu Kyi na kutaka aachiliwe mara moja.

Hata hivyo jeshi la Myanmar limetangaza hali ya hatari ya mwaka mmoja na kusema litafanya uchaguzi mpya mara tu madai yake yatakaposhughulikiwa.

 

AFP/Reuters