1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Profesa Janabi wa Tanzania aula WHO kanda ya Afrika

20 Mei 2025

Profesa Mohamed Yakub Janabi ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika katika Shirika la Afya Duniani (WHO), nafasi anayotarajiwa kuanza rasmi kuishika baada ya kuidhinishwa na Bodi Kuu ya WHO mwezi huu Mei.

Tanzania | Mkurugenzi mpya wa WHO Afrika | Prof. Mohammed Yakub Janabi
Profesa Janabi ni Mtandaji Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili nchini Tanzania.Picha: Eric Boniphace/DW

Katika kikao maalum cha Kamati ya Kikanda ya WHO kwa Afrika kilichofanyika mjini Geneva kabla ya kuanza kwa Mkutano Mkuu wa Afya Duniani, Profesa Mohamed Yakub Janabi kutoka Tanzania alipendekezwa kuwa Mkurugenzi mpya wa WHO Kanda ya Afrika. Uteuzi huu unakuja kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa amechaguliwa awali, Dk Faustine Ndugulile, mnamo Novemba 2024.

Wagombea wengine waliokuwa kwenye kinyang'anyiro hicho ni pamoja na Dk N'da Konan Michel Yao kutoka Côte d'Ivoire, Dk Mohamed Lamine Dramé kutoka Guinea, na Profesa Moustafa Mijiyawa wa Togo.

Mapendekezo ya uteuzi wa Profesa Janabi yatapelekwa kwa Bodi Kuu ya WHO (Executive Board) katika kikao chake cha 157 kitakachofanyika tarehe 28 na 29 Mei 2025 mjini Geneva. Akiteuliwa rasmi, Profesa Janabi ataanza rasmi majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitano, akiwa na nafasi ya kuteuliwa tena kwa muhula mwingine.

Profesa Janabi atahudumu katika nafasi hiyo kwa muhula wa miaka mitano unaoweza kurefushwa.Picha: Eric Boniphace/DW

Katika hotuba yake ya kukubali uteuzi huo, Profesa Janabi alisema: "Asanteni kwa kuniamini. Sitawaangusha. Mshikamano huu unaonyesha dhamira yetu ya pamoja ya kuijenga Afrika yenye afya bora, imara na iliyoungana. Tunakabiliwa na changamoto nyingi – kuanzia magonjwa ya kuambukiza, yasiyoambukiza, hadi mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa fedha za afya – lakini tutazishinda tukitumia mshikamano na ujasiri wa Waafrika."

Pongezi kutoka kwa viongozi wa WHO

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, alimpongeza Profesa Janabi kwa uteuzi huo na pia kutoa shukrani kwa wagombea wengine kwa kampeni zao.

Soma pia: WHO yaufungua mkutano wake wa 78 mjini Geneva

"Nampongeza Profesa Janabi na pia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mafanikio haya. Anaingia katika nafasi hii wakati wa changamoto kubwa kwa Kanda ya Afrika na kwa WHO kwa ujumla. Tunathamini uzoefu wake na tunatarajia kufanya kazi naye kwa ajili ya Afrika yenye afya, usalama na usawa zaidi," alisema Dk Tedros.

Ulaji wa chakula usiofaa chanzo cha matatizo ya afya

03:22

This browser does not support the video element.

Aidha, Dk Tedros alimshukuru Dk Chikwe Ihekweazu, aliyekuwa Mkurugenzi wa muda wa WHO Afrika, kwa uongozi wake katika kipindi cha mpito kufuatia kumalizika kwa muda wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Kanda hiyo, Dk Matshidiso Moeti.

"Hongera Profesa Janabi kwa kuchaguliwa kwako. Hili linaonesha imani kubwa ya nchi wanachama kwako. Kanda ya Afrika imepiga hatua, lakini bado tunakabiliwa na changamoto nyingi. Utaungwa mkono kikamilifu na timu nzima ya WHO Afrika katika kutekeleza jukumu hili muhimu."

Kwa mara nyingine, Tanzania imeandika historia katika ulingo wa kimataifa wa afya kwa kupewa jukumu la kuongoza ajenda ya afya ya bara zima la Afrika kupitia Profesa Janabi — hatua inayokuja wakati ambapo bara hili linahitaji uongozi imara zaidi ya wakati wowote.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW