Jenerali Oligui Nguema ashinda uchaguzi wa Rais Gabon
14 Aprili 2025
Kiongozi wa kijeshi wa Gabon, Brice Oligui Nguema, ametangaza ushindi mkubwa katika uchaguzi wa urais uliofanyika Jumamosi, ambapo matokeo ya awali yalionesha amepata asilimia 90.35 ya kura. Oligui, aliyemaliza utawala wa familia ya Bongo uliodumu kwa zaidi ya miaka 50 mnamo Agosti 2023 na kuwa rais wa mpito, aliahidi kurejesha demokrasia nchini.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Hermann Immongault, alisema Oligui ameshinda kwa kura zaidi ya 575,200, huku mpinzani wake mkuu, Alain-Claude Bilie By Nze, akipata asilimia tatu pekee. Wagombea wengine sita hawakuvuka asilimia moja ya kura.
Soma pia:Mahakama ya Gabon yapitisha majina nane ya wagombea urais
Uchaguzi huu uliitikiwa kwa asilimia 70.4 ya wapiga kura milioni 2.3 wa taifa hilo lenye utajiri wa mafuta. Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa alimpigia simu Oligui kumpongeza kwa ushindi na mwenendo mzuri wa uchaguzi. Tofauti na chaguzi zilizopita za 2016 na 2023 ambazo ziligubikwa na machafuko, mitaa ya mji mkuu Libreville ilikuwa na utulivu baada ya upigaji kura.
Licha ya kuahidi mageuzi, wakosoaji wanamshutumu Oligui kwa kushindwa kuachana na mifumo ya uporaji wa rasilimali chini ya utawala wa kina Bongo, ambao aliutumikia kwa miaka mingi.
Hata hivyo, kampeni yake ilitawala kabisa huku wapinzani wake saba, wakiwemo wanasiasa wa zamani wa utawala wa Bongo, wakiwa hawakuonekana sana. Matokeo ya mwanzo yalionesha Oligui alikuwa akiongoza kwa asilimia 100 katika baadhi ya vituo vya kupigia kura, hatua inayozua maswali kuhusu usawa wa ushindani wa kisiasa nchini humo.