1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto mmoja kati ya sita wanaishi katika mazingira ya vita

Babu Abdalla 13 Februari 2020

Serikali ulimwenguni zimetakiwa kufanya juhudi zaidi kuwalinda watoto kutokana na athari za vita. Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la Save The Children, vita ndio hatari kubwa inayokabili maisha ya watoto.

Somalia Kindersoldaten
Picha: Getty Images/AFP/M. Dahir

Athari ya vita huwapata sio tu walioshiriki katika vita hivyo bali hata wasiohusika. Shirika la Save the Children limesema vita vinaathiri ukuaji mzuri katika maisha ya watoto na pia wanakabiliwa na athari ya kuuawa, kujeruhiwa, kusajiliwa katika jeshi au hata kunyanyaswa kingono.

Katika ripoti yake, shirika hilo limeonyesha kusikitishwa na ukimya wa viongozi duniani wakati watoto wanapitia madhila makubwa katika mazingira ya vita.

Afisa mkuu mtendaji wa Save the Children Inger Ashing amesema kuwa tangu mwaka 2005, watoto wapatao elfu 95 wameuawa na maelfu kutekwa nyara. Athari za vita pia zimesababisha mamilioni ya watoto kukosa nafasi ya kupata elimu na huduma za matibabu.

Inger ameonya kuwa mustakabali wa watoto utaendelea kuwa mashakani iwapo hakutafanyika lolote kuwalinda na pia wanaohusika na kuwafanyia unyama watoto hawatochukuliwa hatua.

"Ni jukumu letu kama viongozi kufanya kila liwezekanalo kulinda watoto, ambao ni mustakabali wetu dhidi ya vurugu na vita ambavyo kamwe haviwahusu. Kwa pamoja, tunaanza kupiga hatua lakini tunahitaji kuwa na dhamira moja", amesema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Ripoti hiyo inasema kuwa mnamo mwaka 2018, angalau mtoto mmoja kati ya sita kote duniani, ambao ni watoto takriban milioni 415, waliishi katika mazingira ya migogoro. Takwimu hizo ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya mwaka 1995.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa matukio ya ukiukwaji wa haki za watoto yaliongezeka kwa asilimia 170 tangu mwaka 2010. Aidha watoto wa Kiafrika ndio walioathirika zaidi wakati takwimu zikionyesha kuwa watoto milioni 170 wanaishi katika mazingira ya vita japo watoto wanaoishi katika eneo la Mashariki ya kati pia wameathirika na vita vinavyoendelea sehemu hizo. 

Ripoti ya Save the Children inaonyesha kuwa wavulana wadogo husajiliwa kama majeshi

Wavulana waliosajiliwa katika jeshi wakati wa zoezi la kurudisha silaha Sudan KusiniPicha: Getty Images/AFP/C. Lomodong

Yamkini mataifa yaliotajwa kuwa na mazingira mabaya zaidi kwa watoto kuishi ni Afghanistan, ikifuatiwa na Jamhuri ya Afrika ya kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Iraq na Mali.

Ripoti hiyo imeweka wazi kuwa wasichana hupitia ukatili wa kijinsia, au hata kulazimishwa kuolewa wakiwa wangali wadogo huku nao wavulana wakitekwa nyara na kusajiliwa kama majeshi.

Samira ambaye ni msichana wa miaka 15 kutoka Iraq, licha ya umri wake mdogo ameanza majukumu ya ulezi wa mtoto wake wa miaka miwili. Msichana huyo alitekwa nyara mnamo mwaka 2016 na baadaye kuuzwa kama mtumwa na hatimaye kuozwa kwa lazima kwa mpiganaji wa kundi la dola la Kiislamu la Islamic State.

 

Vyanzo AFP