1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtoto wa Gaddafi ajitosa rasmi kuwania urais Libya

Sylvia Mwehozi
14 Novemba 2021

Mtoto wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi, Seif al- Islam ametangaza rasmi nia yake ya kuwania urais katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Desemba.

Libyen Sebha | Saif al-Islam al-Gaddafi registriert sich als Präsidenstchaftskandidat
Picha: Khaled Al-Zaidy/REUTERS

Seif al- Islam al-Gaddafi mwenye umri wa miaka 49, amejitokeza na kuonekana katika mkanda wa vidio uliotolewa na ofisi inayosimamia uchaguzi, akitia saini nyaraka katika kituo cha uchaguzi kusini mwa mji wa Sebha. Kwenye vidio hiyo Seif amesema Mungu pekee ndiye ataamua juu ya mustakabali wa taifa hilo.

Seif al-Islam ni mmoja wa watu mashuhuri na mwanasiasa mwenye utata anayetarajiwa kuwania urais. Baadhi ya wagombea wengine ni pamoja na kamanda wa kijeshi upande wa mashariki Khalifa Haftar, waziri Mkuu Abdulhamid al-Dbeibah na spika wa bunge Aguila Saleh.Miaka 10 tangu Gaddafi kuuawa, Libya ingali inayumba

Hata hivyo, wakati jina lake ni miongoni mwa majina yanayojulikana sana Libya, na miongoni mwa watu waliokuwa na jukumu kubwa katika sera za nchi hiyo kabla ya vuguvugu la mwaka 2011 lililoungwa mkono na Jumuiya  ya kujihami NATO na kuharibu utawala wa familia yake, Seif amekuwa nje ya macho ya umma kwa karibu muongo mmoja.

Kujitosa kwake rasmi katika kinyang'anyiro cha uchaguzi, ambao sheria zake bado zinazozaniwa na makundi tofauti ya Libya, kunaibua hoja mpya ya uchaguzi utakaomshirikisha mgombea anayetizamwa katika baadhi ya mikoa kuwa asiyekubalika.

Seif al-Islam mwaka 2008 kabla ya utawala wa baba yake kuangushwaPicha: MAHMUD TURKIA/AFP/Getty Images

Licha ya umma wa Libya na mataifa ya kigeni kuunga mkono uchaguzi wa Desemba 24, kura hiyo imesalia mashakani kwasababu ya kutokubaliana juu ya kanuni na ratiba ya uchaguzi.

Mkutano mkubwa juu ya Libya uliofanyika Paris wiki iliyopita, ulikubaliana juu ya kuweka vikwazo kwa yeyote atakayeingilia kura hiyo, lakini ikiwa zimebaki wiki sita kabla ufanyike, hakuna makubaliano yaliyofikiwa juu ya sheria za uchaguzi.

Changamoto nyingine ni pamoja na mpasuko mkubwa baina ya eneo la mashariki na magharibi, mgawanyiko uliotokana na vita ya muda mrefu na uwepo wa maelfu ya wapiganaji na mamluki wa kigeni.

Seif al-Islam alikamatwa na wapiganaji mwishoni mwa mwaka 2011, mwaka ambao baba yake aliondolewa madarakani kabla ya kuuwawa. Aliachiwa mnamo mwezi Juni mwaka 2017, baada ya kuwekwa kizuizini kwa zaidi ya miaka mitano.

Kwa muda mrefu kumekuwa na uvumi juu ya uwezekano wa Seif kujitosa katika mbio za urais.Seif al-Islam anatakiwa na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita dhidi ya makosa ya ubinadaamu yanayodaiwa kufanywa wakati wa mapinduzi ya mwaka 2011.

Vyanzo: Reuters/AP/AFP