Mtoto wa mwaka mmoja apona saratani ya damu
9 Novemba 2015Laylah Richard mwenye umri wa mwaka mmoja, alikuwa akisumbuliwa na saratani ya damu, lakini amepona baada ya wanasayansi kutumia mbinu mpya ya vinasaba vilivyorekebishwa ili kuzifanyia kazi chembechembe za kupambana na ugonjwa huo, katika hospitali ya Great Ormond Street-GOSH, iliyopo katikati ya mji wa London.
Profesa Paul Veys, mkurugenzi wa kupandikiza uboho wa mfupa katika hospitali ya GOSH na daktari mkuu wa Laylah amesema kutokana na hii kuwa mara ya kwanza tiba hiyo kutumika, hawakujua kama itafanya kazi, hivyo wamefurahi sana baada ya kuona imeweza kufaulu.
Profesa Veys amesema saratani ya mtoto huyo ilikuwa katika kiwango kibaya, hivyo matokeo hayo ni sawa na muujiza. Mtoto huyo aligunduliwa na aina ya saratani ya damu ya Lymphoblastic, ambayo hutokea sana utotoni, wakati akiwa na wiki 14.
Laylah ambaye madaktari walidhani huenda atakufa, alipatiwa tiba ya kutumia kemikali na alipandikiziwa uboho wa mfupa, lakini saratani hiyo ikarejea tena na ndipo madaktari wakawaelezea wazazi wake kufikiria mtoto wao kupatiwa tiba ya kupunguza maumivu.
Familia ilipewa muda wa kuamua
Familia yake kisha ikapewa nafasi ya mtoto kufanyiwa matibabu ya majaribio katika hospitali hiyo, ambapo madaktari walirekebisha chembechembe nyeupe za damu na chembechembe za T, kutoka kwa mfadhili ambaye afya yake imeimarika, ili waweze kuzisaka na kuziua chembechembe sugu ambazo zinasababisha saratani ya damu.
Baba wa mtoto huyo, Ashleigh Richards, mwenye umri wa miaka 30, amesema Laylah alikuwa akipata maumivu makali, hivyo iliwabidi watafute njia ya kumuondolea maumivu hayo.
Mtoto huyo aliwekewa dripu ya chembechembe zinazojulikana kama UCART 19. Wiki chache baadae, madaktari wakaeleza kuwa dawa hiyo imefanya kazi.
Madaktari wamesisitiza kuwa matibabu hayo yametumika mara moja na kwamba matokeo yake yatahitaji kurudiwa, lakini amesema majaribio hayo yanaonyesha kufanikiwa.
Waseem Qasim, Profesa wa chembechembe na tiba ya vinasaba katika taasisi ya watoto na mshauri wa elimu ya kinga ya maradhi katika hospitali ya GOSH, amesema wameitumia tiba hiyo kwa mtoto mdogo sana, hivyo iliwapasa kuwa makini kuhusu madai kwamba tiba hiyo itafaa kwa matibabu ya watoto wote.
Profesa Qasim amesema majaribio hao yameonyesha kupigwa kwa hatua moja mbele katika kuitibu saratani ya damu pamoja na saratani nyingine.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE
Mhariri: Daniel Gakuba