1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtu mmoja afa kwa virusi vya Corona Italia

22 Februari 2020

Mwanaume mmoja wa Italia aliyekuwa ameathirika na virusi vya Corona amefariki dunia na hivyo kifo hicho kuwa cha kwanza kutokea barani Ulaya tangu virusi hivyo vilipozuka China na kusambaa ulimwenguni.

Italien Codogno Coronavirus
Picha: picture-alliance/AP/L. Bruno

Waziri wa Afya wa Italia, Roberto Speranza amesema mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 78, alifariki siku ya Ijumaa kwenye hospitali ya mji wa Padua, alilokuwa amelazwa kwa siku 10. Speranza amesema mwanaume huyo alikuwa miongoni mwa watu wawili waliokutwa na virusi vya Corona vinavyojulikana kama COVID-19 katika mkoa wa Veneto.

Madaktari watano na wauguzi pamoja na wagonjwa kadhaa wameambukizwa virusi hivyo katika hospitali ya Codogno ambako mgonjwa huyo alikuwa akitibiwa. Watu wengine watatu ambao walikwenda kwenye mgahawa mmoja kwenye mkoa wa Lombardy, walithibitika kuugua virusi vya Corona.

Kuzuia mripuko

Maafisa wa Italia wameamuru kufungwa kwa shule, majengo ya umma pamoja na migahawa kwenye miji 10 ya kaskazini mwa nchi hiyo baada ya visa vingine 15 kuripotiwa. Visa vyote hivyo vimeripotiwa kwenye mkoa wa Lombardy, ambako mwanaume mwenye umri wa miaka 38 aliugua virusi vya Corona baada ya kukutana na mtu aliyerejea kutoka China mwishoni mwa mwezi Januari.

Maafisa wa afya wa Italia wamesema kuwa mamia ya watu wamewekwa katika karantini na wanachunguzwa iwapo wameambukizwa virusi hivyo ama la. Zaidi ya watu 150 wanaofanya kazi na mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 38 pamoja na maafisa 70 wa afya katika hospitali ya Codogno ni miongoni mwa watu ambao wanachunguzwa.

Watu wakitembea kwenye mtaa usio na watu katika kijiji cha Codogno, ItaliaPicha: Reuters/Local Team

Wakati huo huo, Korea Kusini imeripoti visa vipya 142 vya Corona na kuifanya idadi jumla ya walioambukizwa virusi hivyo nchini humo kufikia 346, hizo zikiwa ni takwimu zilizotolewa siku ya Jumamosi. Nchi hiyo pia imeripoti kifo cha pili kinachotokana na virusi vya Corona.

Waziri Mkuu wa Korea Kusini, Chung Sye-kyun ameitaja hali hiyo kuwa ya dharura. Miji ya Daegu na Cheongdo imeteuliwa kuwa na maeneo maalum kwa ajili ya kuwaangalia wagonjwa wa virusi vya Corona.

Maambukizi yapungua China

Huku idadi ya maambukizi ikiongezeka mara mbili Korea Kusini, idadi ya maambukizi imepungua China hadi 397. Takwimu hizo zimetolewa siku ya Jumamosi na Tume ya Afya ya Taifa ya China. Idadi ya watu waliokufa kutokana na virusi vya Corona China bara imefikia 2,345 baada ya vifo 109 kuongezeka siku ya Ijumaa na walioambukizwa ni 76,288. Takwimu hizo mpya zimepungua ikilinganishwa na zilizotolewa siku ya Ijumaa ya visa vipya 889.

Iran pia inapambana kuvidhibiti virusi vya Corona ndani ya mipaka yake. Siku ya Ijumaa maafisa walitangaza kuwepo kwa visa vipya 13 pamoja na vifo viwili vilivyotokana na virusi hivyo. Visa vingi vimeripotiwa kwenye mji mtakatifu wa Qom, ingawa kuna watu wengine ambao wameambukizwa pia kwenye miji mingine.

Lebanon kwa upande wake imeripoti kisa cha kwanza, baada ya mwanamke mwenye umri wa miaka 45 kuthibitika kuambukizwa virusi vya Corona. Imeelezwa kuwa mwanamke huyo hivi karibuni aliuzuru mji wa Qom.

Maafisa wa Korea Kusini wakinyunyizia dawa ya kujikinga na virusi vya Corona kwenye mji wa DaeguPicha: picture-alliance/AP Photo/K. Jun-boem

Aidha, maafisa wa Israel wamethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya Corona kutoka kwa abiria aliyekuwa ndani ya meli ya ya kifahari ya Diamond Princess. Awali wakati anawasili Israel, mtu huyo alionekana hajaambukizwa virusi hivyo.

Shirika la Afya Duniani, WHO, limesema kuwa idadi jumla ya watu walioambukizwa virusi vya Corona ulimwenguni imefikia 77,000.

Uingereza yawarejesha raia wake waliokwama kwenye meli Japan

Ama kwa upande mwingine, serikali ya Uingireza Jumamosi imeanza kuwaondoa raia wake kutoka kwenye meli ya Diamond Princess baada ya kuwekwa chini ya karantini kwa zaidi ya wiki mbili mjini Yokohama, Japan kutokana na kushambuliwa na virusi vya Corona.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Uingereza imeeleza kuwa ndege ya kuwarejesha nyumbani raia wake imeshaondoka Japan ikiwa na abiria 32 wa Uingereza na wa nchi nyingine za Ulaya. Ndege hiyo inatarajiwa kuwasili Uingereza asubuhi ya Jumamosi.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara, ndege hiyo itatua kwenye kambi ya jeshi ya Boscombe Down kusini mwa Uingereza na abiria wote watawekwa nchini ya karantini kwa siku 14 zaidi.

Mamia ya abiria waliruhusiwa wiki hii kuondoka katika meli hiyo baada ya kuonekana hawajaambukizwa virusi vya Corona. Marekani, Canada, Australia, Korea Kusini na Hong Kong zote zimesema zitawaondoa raia wake kutoka kwenye meli hiyo, huku zaidi ya Wamarekani 300 wakirejea nyumbani siku ya Jumatatu.

(AFP, DPA, AP, Reuters, DW https://bit.ly/2PfFvzK)

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW