1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAfghanistan

Afghanistan yakubwa na tetemeko jingine la ardhi

12 Oktoba 2023

Afganista imekabiliwa na tetemeko jengine la ardhi lenye ukubwa wa 6.3 kipimo cha richter katika mkoa wa Herat, magharibi mwa Afghanistan.

BdTD | Afghanistan, Herat | Suche nach Vermissten nach den Erdbeben
Picha: Ebrahim Noroozi/AP/picture alliance

Tetemeko hilo limesabisha kifo cha mtu mmoja na kuongeza hofu miongoni mwa wakazi  kutokana na mfululizo wa matetemeko yaliwauwa takriban watu 2,000 mwishoni mwa juma. 

Soma pia: Tetemeko la Ardhi laua watu zaidi ya 2000 Afghanistan

Kulingana na meneja wa gari la kusafirisha wagonjwa katika mkoa wa Herat Abdul Zahir Noorzai tetemeko hilo limesababisha majeraha kwa watu 120 baada ya kuangukiwa na vifusi walipokuwa wamelala nje ya nyumba zao zilizoharibiwa na matetemeko.

Wakazi wengi wamepiga kambi katika mahema, magari na bustani tangu tetemeko la Jumamosi la kipimo cha 6.3 na mfululizo wa matetemeko mengine mabaya.

Wafanyakazi wa kujitolea wamekuwa wakifukua chini ya vifusi kujaribu kuwaokoa  manusura na kuopoa miili ya watu baada ya matetemeko ya awali kuharibu kabisa  takriban vijiji sita katika wilaya ya Zenda Jan. Kulingana na Umoja wa Mataifa zaidi ya watu 12,000 wameathiriwa na mkasa huo.

Hata hivyo maafisa wa serikali za mitaa na kitaifa wametoa hesabu zinazokinzana za idadi ya waliofariki na kujeruhiwa, lakini wizara ya maafa imesema watu 2,053 walifariki.

Soma pia: UN: Kuwarejesha kwa nguvu raia wa Afghanistan kutoka Pakistan kutasababisha mgogoro

Kaimu Waziri wa Afya ya Umma wa Afghanistan Qalandar Ebad amesisitiza hitaji la msaada wa dharura kwa waathiriwa. 

"Tunahitaji vifaa vya dharura na dawa na pia matibabu ya msaada kwa wagonjwa hawa wote. Tumejaribu na.. wamefanya mambo mengi.Lakini kwa muda mrefu, kama tunavyojua kwamba baada ya maafa, kuna magonjwa ya kuambukiza. Kuna uhaba wa maji hasa maji safi ya kunywa na pia hali ya usafi sio nzuri. Pia suala la lishe, hili ni jambo kubwa na ni changamoto kwetu. Labda tutakabiliwa na magonjwa mengi ya kuambukiza. Kwa sababu hakuna makazi kwa waathiriwa na kukosekana pia kwa maji safi." amesema Qalandar Ebad.

Ahadi za misaada

Mkoa wa Herat magharibi mwa AfghanstanPicha: ALI KHARA/REUTERS

Mataifa na mashirika mbali mbali yameahidi kuisaidia Afghanistan, huku Umoja wa Ulaya ukiahidi msaada wa euro milioni 3.5  katika ufadhili wa dharura na kuongeza mgao mpya wa euro milioni 2.5 kwa mashirika wa kibinadamu ambayo tayari yanaendeleza shughuli za misaada nyanjani.

Pakistan, Iran na China zimeahidi kutuma chakula, mablanketi, dawa, mahema na fedha. Huku Ofisi ya wizara ya mambo ya nje ya Uturuki ikisema iko tayari kutoa msaada katika juhudi za uokoaji katika maeneo yaliyoathirika.

Afghanistan mara nyingi hukumbwa na matetemeko mabaya ya ardhi, lakini maafa ya wikendi iliyopita yalikuwa mabaya zaidi kuikumba nchi hiyo iliyoharibiwa na vita katika zaidi ya miaka 25.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW