1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mtu na Mazingira

20 Oktoba 2003

Vita Vinachochea Hali Mbaya ya Mataifa Masikini, Unasema Umoja wa Mataifa

Karibuni katika makala nyingine ya Mtu na Mazingira kutoka Redio Deutsche Welle Bonn, Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani. Ni Shaaban Mohamed nikiwatakia usikilizaji mzuri. Kuongezeka kwa migogoro ya kijeshi na migongano ya kiraia katika sehemu za Eshia, Afrika na Amerika ya Kusini, kumechochea shida za mataifa masikini duniani, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mjini New York. "Kwa kawaida migogoro inajisambaza katika nchi masikini: zaidi ya nusu ya nchi zote zenye mapato ya chini zimekuwa na uzoefu wa migoro mikubwa tangu mwaka 1990," unasema uchunguzi wa kurasa 90 wenye kichwa cha maneno 'Hali ya Kijamii Duniani Mwaka 2003'. Mnamo miongo miwili iliyopita ya karne ya 20, kulitokea migogoro 164 ya utumiaji wa nguvu kila pembe ya dunia, na kuziathiri nchi 89 kwa muda wa miaka sita hadi saba kwa wastani.

"Athari kubwa kabisa ilitokea barani Afrika, ambako karibu kila nchi ilipambana na mgogoro mkubwa mnamo mwongo uliopita," ilisema ripoti, ambayo iliwasilishwa katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Nchi zilizoteseka na mapambano ya kijeshi au vita vya kiraia ni pamoja na Sudan, Liberia, Sierra Leone, Somalia, Msumbiji, Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) , Ethiopia na Eritrea. Na kule ambako migogoro inatokea, maendeleo ya kiuchumi yanazuilika, kwa sababu viwanda vinabomolewa, huduma za jamii zinaepukwa, maeneo ya kilimo yanahamwa na wakazi ambao tangu hapo masikini wanakabiliwa na kitisho cha msiba wa njaa. "Miongo iliyopita imeshuhudia pia badiliko la aina za migogoro, pakishuhudiwa uwezekano zaidi wa kutokea mgogoro ndani ya nchi badala ya kati ya mataifa," unsema uchunguzi.

Nchi kama Siera Leone, Liberia na DRC, wale wanaopambana wanadhibiti mali ya raia na maliasili ya kimaubile, pamoja na almasi na mbao. Majeshi matano ya kigeni --kutoka Rwanda, Uganda, Namibia, Zimbabwe na Angola --yamekuwa yakihusika mara kadha na vita vya kiraia ama nchini DRC kwa muda wa miaka sita au katika kupora madini au yote mawili. Maliasili nchini -- pamoja na dhahabu, shaba, coltan, almasi, mbao na kobalti -- imekuwa ikiporwa na vikundi vya waasi walioingia vitani. Mapato haramu baada ya kuuzwa madini hizo, hutumiwa kununulia silaha ndogo ndogo na kubwa ambazo zinatumiwa katika migogoro yao. "Uchumi mpya wa vita umesababisha kuundwa vikundi vyenye silaha vikiwa na uongozi hafifu na mipaka inayolindwa. Na matokeo yake ni kujiri mapigano katika miaka michache iliyopita, bila ya kujali mikataba ya Geneva, ambayo ina vifungu pia juu ya kuwahami raia," ripoti iliendelea kusema.

Mizozo ya kijeshi inayoendelea katika nchi kama India na Pakistan, Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini, imezisababisha nchi hizo za Eshia kuongeza matumizi ya kijeshi -- kwa gharama ya maendeleo ya kiuchumi. Akiihotubia Kamati ya Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama na Kuvuliwa Silaha Duniani, Balozi Dumisani Kumalo kutoka Afrika Kusini, aliwaambia wajumbe hivi karibuni, kwamba migogoro ya kijeshi duniani kustawisha ukusanyaji silaha kila pembe ya dunia. "Gharama ya kijeshi duniani, zinatarajiwa kuongezeka hadi Dolla trillioni mwaka huu," aliongeza kusema, "huku nusu ya dunia inateseka kwa umasikini wa kudumu." Katika ripoti yake ya kila mwaka katika mwezi wa Juni, Taasisi ya Utafiti wa Amani Duniani yenye makao yake mjini Stockholm, ilisema gharama za matumizi ya kijeshi ziliongezeka kwa kadiri kubwa mwaka jana -- hadi Dolla bilioni 784 ukilinganisha na Dolla bilioni 741 mwaka 2001.

Kwa mujibu wa Tarakimu za Maendeleo Duniani mwaka huu, ambazo zilichapishwa na Benki ya Dunia, umasikini unaopimwa kwa mapato, umejisambaza kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika. Kwa wastani asilimia 51 ya watu kaidri ya milioni 324 wanaishi kwa msaada wa chini ya Dolla moja kwa siku. Na Eshia ya Kusini ina wakazi wengi kabisa duniani ambao wanaishi chini ya kiwango cha umasiki, kadiri ya asilimia 40 au kadiri ya watu milioni 437. Hivi sasa kuna watu kadiri ya bilioni 1.2 ambao wanaishi katika hali mbaya kabisa ya umasikini. Ripoti inachunguza vikundi vya jamii, pamoja na watu wazima, vijana, wale wasiojiweza, wenyeji asilia, wahamiaji na watu wanaojikuta katika migogoro na kuzingatia masuala ya kijinsia.

Katika mkutano mkuu wa milenia mwaka 2000, viongozi wa dunia waliahidi kupunguza hadi nusu jumla ya watu wanaoishi katika hali ya umasikini hadi mwaka 2015. Lakini jumuia ya kimataifa haitarajiwi kufikia lengo hilo, kutokana na sababu kadha, miongoni mwao kupungua msaada wa maendeleo, kuongezeka madeni duniani, kujisambaza Ukimwi na migogoro ya kijeshi na dhila za kiraia. Kwa upande mwingine, mnamo wakati ambao kila dakika moja anauawa mtu kwa bunduki duniani, vikundi vya usalama hivi karibuni vilianzisha kampeni juu ya kutayarishwa mkataba unaopiga marufuku biashara ya silaha isiyokagulika duniani. "Silaha ndogo ndogo ni kitisho kipya cha kuwangamiza wanaadamu," alisema Bibi Rebecca Peters, mkuu wa Mtandao wa Kimataifa unaohusika na Silaha ndogo ndogo, ambao umeviweka mahala pamoja vikundi 550 katika nchi 100.Mtandao huo, pamoja na Amnesty International na kikundi cha msaada Oxfam, vilianzisha kampeni mijini Lima, Nairobi na London.

Silaha ndogo ndogo zinawaua watu nusu milioni kwa mwaka, alisema Peters, na kuna silaha kama hizo milioini 650 mikononi mwa watu -- moja kwa kila watu kumi duniani. Asilimia 70 ya silaha hizo zimo mikononi mwa raia wa kawaida. "Hili ni jamo ambalo haliwaziki. Raia wa kawaida wana silaha nyingi zaidi kuliko askari wote na polisi wote duniani," alisema Peters. Kampeni hiyo, ambayo inageukia silaha ndogo ndogo, zinazonunuliwa na watu kinyume cha sheria au makundi ya wahalifu, na kujitafutia mkataba wa kimataifa kuzuia biashara ya silaha hizo,alisema Peters. Marekani ina silaha milioni 200, karibu thuluthi moja ya jumla ya dunia nzima, lakini biashara ya madawa ya kulevya na viwango vinavyopanda vya uhalifu mijini, yote hayo yanazidisha tatizo la silaha katika Amerika Kusini. Benki ya Maendeleo ya Amerika inakadiria kwamba gharama yake ni Dolla bilioni 170 kwa mwaka. Nchini Colomba, msafirishaji mkubwa kabisa kokein duniani ikijikuta katika vita vya ndani kwa muda wa miongo minne, ubora wa mhakawa unaweza kuthaminiwa kwa jumla ya walinzi wake wenye silaha. Wakolombia matajiri wanaishi katika ngome wakiwa na walinzi wenye silaha. Katika sehemu za mashambani mabwana vita wanatembea mchana na bastola kiukononi ,na hata mashingani. Silaha ndogo ndogo zilisababisha vifo vya watu 40,000 nchini Brazil mwaka jana, kulingana na tarakimu rasmi. Umoja wa Mataifa unasema, nchi hiyo inashuhudia asilimia 11 ya mauaji ya bunduki, kiwango cha juu kabisa duniani. Wataalamu wanasema wakazi wengi wa Amerika ya Kusini wanahisi kwamba wamelazimika kujihami, kwa sababu umasikini umepunguza jumla ya polisi. Kwa mujibu wa uchunguzi wa Umoja wa Mataifa, silaha ndogo ndogo laki moja zinaibiwa kila mwaka duniani.


Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW