1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroRwanda

Mtuhumiwa mauaji ya kimbari Rwanda kufikishwa Mahakamani

14 Novemba 2023

Kumekuwa na shinikizo linaloongezeka nchini Ufaransa ili kuwawajibisha wote wanaohusika katika kesi ya mauaji ya halaiki nchini Rwanda. Daktari mmoja raia wa Rwanda anakabiliwa na kesi itakayosikilizwa mjini Paris.

Kigali Völkermord Memorial
Rais wa Rwanda Paul Kagame na mkewe Jeannette Kagame wakiwasha mwenge wa kumbukumbu ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika jumba la makumbusho la Gisozi mjini Kigali: 07.04.2023Picha: Mariam Kone/AFP/Getty Images

Raia wa Rwanda na daktari wa magonjwa ya wanawake Sosthene Munyemana, ambaye anatuhumiwa kuhusika katika mauaji ya watu wengi katika jimbo la Butare, kusini mwa Rwanda, ambalo kwa sasa linafahamika kama Huye, atafikishwa mahakamani siku ya Jumanne (14.11.2023) mjini Paris. Hii ni kesi ya saba inayoendelea nchini Ufaransa kuhusiana na mauaji ya kimbari ya Rwanda. Upande wa mashitaka wanaielezea kama kesi yenye umuhimu mkubwa.

Mauaji ya huko Butare yalianza karibu wiki mbili baada ya kuuawa kwa rais Habyarimana. Inakadiriwa kuwa zaidi ya watu 200,000 waliuawa wakati huo. Mshtakiwa, Sosthene Munyemana, ambaye sasa ana umri wa miaka 68, ni Mhutu ambaye aliishi Butare wakati huo na alikuwa daktari wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya chuo kikuu.

Wahutu wakiwapokea wanajeshi wa Ufaransa Julai 3,1994 wakati wakipita katika kambi ya wakimbizi takriban kilometa 4 nje kidogo ya mji wa Butare huko Rwanda. Ufaransa umekuwa ikituhumiwa kuwa na jukumu katika mauaji hayo ya kimbari.Picha: dpa/picture alliance

Munyemana amejitetea kuwa aliondoka Rwanda katikati ya mwezi Juni mwaka 1994, akielekea kwanza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kisha Ufaransa. Ni baba wa watoto watatu na ameishi Ufaransa na familia yake tangu wakati huo. Amekuwa akifanya kazi tangu mwaka 2001 kama daktari wa magonjwa ya wanawake katika hospitali ya Saint-Cyr kusini magharibi mwa mji wa Villeneuve-sur-Lot.

Mauji ya kimbari: Ushirikiano au kutodhamiria?

Daktari huyo sasa anatuhumiwa kushiriki katika mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Ashutumiwa kushiriki katika maandalizi na utendaji wa uhalifu huo. Pamoja na watu wengine mashuhuri wa eneo hilo, inasemekana alitia saini barua inayoiunga mkono serikali ya mpito ambayo ilipanga  mauaji ya kimbari.

Inasemekana Munyemana alichaguliwa katika kamati ya kuhusika na mgogoro huo ambayo iliweka vizuizi barabarani ili kuwasaka Watutsi. Pia anashutumiwa kwa kuwafungia watu katika mazingira ya kinyama katika ofisi za serikali za mitaa huku akihodhi funguo na kusaidia katika usafirishaji wa watu wao.

Lakini wakili wa Munyemana, Jean-Yves Dupeux, anakanusha shutuma hizo . Anasema barua hiyo iliandikwa Aprili 16, wakati ambapo mauaji yalikuwa bado hayajaanza huko Butare. Wakili Dupeux ameiambia DW kuwa mteja wake alidhani serikali hiyo ya mpito ingeliweza kuzuia vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Wakili wa mtuhumiwa wa mauaji hayo ya kimbari (Munyemana): Jean-Yves Dupeux.Picha: Privat

Zaidi ya hayo, wakili huyo amesema ingawa  Munyemana  alishiriki katika mkutano wa Aprili 17, 1994, hakuchaguliwa katika nafasi yoyote iliyo rasmi, na kwamba madhumuni ya kamati hiyo ilikuwa kujaribu kuzuia mauaji. Amesema pia kuwa Munyemana alipokea funguo za ofisi ya serikali ya mtaa mnamo Aprili 23 ili aweze kuwaficha baadhi ya watu huko ili kuzuia wasiuawe.

Wakili Jean-Yves Dupeux amesema utawala wa sasa wa Rwanda unawashinikiza watu kadhaa kutoa ushahidi dhidi ya mteja wake, kwa sababu tu anaweza kuwa kiongozi wa upinzani. Amehitimisha kuwa ripoti ya hivi majuzi ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, inabainisha kuwa utawala wa Rwanda unafanya kila uliwezalo ili  kuwanyamazisha kwa njia zote wapinzani watarajiwa wanaoishi nje ya nchi.

Historia fupi ya mauaji ya kimbari Rwanda

Baadhi ya mafuvu ya watu waliouawa katika mauaji hayo ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.Picha: Ben Curtis/AP/picture alliance

Aprili 6, mwaka 1994, ni siku ambayo haitosahaulika katika historia ya Rwanda. Jioni ya siku hiyo, rais wa wakati huo Juvenal Habyarimana alikuwa akirejea kutoka nchi jirani ya Tanzania wakati ndege yake ilipokuwa ikijaribu kutua katika uwanja wa mji mkuu Kigali ilipodunguliwa na kombora. Abiria wote wa ndege hiyo walikufa, akiwemo rais wa Burundi Cyprien Ntaryamira.

Wahusika wa shambulio hilo hadi sasa bado hawajafahamika. Hata hivyo, tukio hilo linazingatiwa kuwa kichocheo cha mauaji ya kimbari yaliyodumu kwa muda wa miezi mitatu, ambapo  inakadiriwa watu 500,000 hadi milioni 1 waliuawa.

Rais Habyarimana alikuwa kutoka kabila la walio wengi nchini Rwanda la Wahutu. Watutsi walio wachache wanatuhumiwa kutekeleza mauaji ya rais huyo, ambayo yalifuatiwa na mauaji ya halaiki yaliyo walenga Watutsi na Wahutu wenye msimamo wa wastani.

(Taarifa hii imeripotiwa na mwandishi wa DW mjini Paris Lisa Louis.)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW