Mtuhumiwa wa ugaidi, Ahmed Ghailani, mahamani mjini New York
10 Juni 2009Mfungwa wa mwanzo aliyekuweko katika gereza la Kimarekani la Guantanamo na aliyehamishiwa kushtakiwa mbele ya mahakama ya kiraia huko Marekani jana alikataa kuwa ana hatia ya kushiriki katika kushambuliwa kwa mabomu balozi za Marekani katika miji ya Nairobi na Dar es Salaam hapo mwaka 1998, visa vilivosababisha vifo vya watu 224. Mtanzania Ahmed Khalfan Ghailani alishikilia hana hatia pale jaji wa mahakama mjini New York alipomsomea mashtaka.
Ahmed Khalfan Ghailani amekuweko katika gereza la Guantanamo tangu mwaka 2006 kwa mashtaka ya kushiriki katika mashambulio hayo. Huenda akakabiliwa na adhabu ya kifo pindi atapatikana na hatia.
Kesi hiyo ni hatua ya kwanza katika mpango wa Rais Obama wa kutaka kuifunga jela ya Guantanamo na kuwahamisha wafungwa wote waliobakia huko kuwapeleka mbele ya mahakama za Marekani au kuwarejesha makwao. Ahadi ya kuifunga jela ya Guantanamo ilikuwa moja wapo ya ahadi alizotoa Rais Obama wakati wa kampeni zake za uchaguzi mwaka jana, pamoja na pia kuachana na mtindo wa kuwatesa wafungwa.
Tulimuuliza Profesa Chris Peter, mwanasheria na mwanaharakati wa haki za binadamu huko Tanzania, kwamba sasa Ahmed Khalfan Ghailani ameipuka kupelekwa mbele ya mahakama ya kijeshi huko Guantanamo na badala yake sasa anashtakiwa mbele ya mahakama ya kiraia ya New York, kuna afuweni kwake:
Wakili mkuu wa serekali ya Marekani, Eric Holder, anasema kuhamishiwa Ahmed Khalfan Ghailani hadi New York kutasaidia kupatikana haki na hakutakuwa ni kitisho kwa Marekani. Alisema idara ya sheria ya huko Marekani ina historia refu ya kuwashtaki washukiwa wa ugaidi kupitia mfumo wa mahakama za jinai, na uzoefu huo utatumiwa katika kutafuta haki kwenye kesi hii.
Ahmed Khalfan Ghailani anakabiliana na makosa 286 ya mauaji, njama ya kuuwa, kushambulia kwa mabomu na kuwajeruhi watu, pamoja na kufanya njama za kutumia silaha za maangamizi dhidi ya raia wa Kimarekani. Pia imetajwa kwamba Ghailani alifanya njama na kiongozi wa mtandao wa al-Qaida, Osama Ben Laden, kuwauwa Wamarekani.
Inasemakana pia kwamba baadhi ya wafungwa wa Guantanamo itakuwa shida kuwashtaki kwa vile ushahidi dhidi yao hautakubalika mahakamani kwa vile umepatikana baada ya kuhojiwa washukiwa kwa kutumiliwa nguvu, jambo ambalo wahakiki wanasema ni mateso. Lakini baadhi ya wafungwa hao itaonekana kuwa ni hatari kuwaacha huru kabisa.
Haifikiriwi kwamba ushahidi wa kabla uliopatikana katika mahojiano ya huko Guantanao, na unaoshukiwa umepatikana kwa kubinywa washukiwa utakubaliwa uzungumziwe katika mahakama ya kiraia.
Kwa upande mwengine, Ikulu ya Marekani imekataa kusema kama Ahmed Khalfan Ghailani ataachiwa huru pindi mahakama ya New York itamkutana hana hatia.. Msemaji wa Ikulu ya Washington , Robert Gibbs, alisema hatozungumzia mambo ya dhana, atazungumzia kama jambo hilo litatokea.
Mwandishi:Othman Miraji/RTR/AFPE
Mhariri:M.Abdul-Rahman