1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muandamanaji anayechoma Quran Sweden na historia yake tata

Cathrin Schaer Iddi Ssessanga
22 Julai 2023

Baada ya Salwan Momika kupamba vichwa vya habari vya kimataifa kwa maandamano mjini Stockholm ambapo alichoma Quran, Wairaki wenzake wamesaidia kufichua historia yake ya kisiasa. Msukumo wake unatiliwa shaka.

Pakistan | Proteste - Koran Verbrennung in Schweden
Picha: ARIF ALI/AFPGetty Images

Matendo yake yameibua mzozo mkubwa wa kidiplomasia kati ya Irak na Sweden wiki hii, na pia yanaonekana kusababisha maandamano yanayoendelea katika ulimwengu wa Kiislamu. Lakini ni vigumu kujua ni kwa uzito gani wa tunaweza kuchukulia msukumo wa muomba hifadhi wa Irak, ambaye amechoma hadharani kurasa za kitabu kitakatifu cha Uislamu, Quran, mjini Stockholm.

Salwan Momika, 37, alikuwa amepanga maandamano mengine kwa wiki hii ambapo alisema angechoma Quran.

Hii ilikuja chini ya mwezi mmoja baada ya Muiraki huyo, ambaye amekuwa nchini Sweden tangu 2018, alikuwa tayari amesababisha kilio cha kimataifa mwishoni mwa Juni wakati alipochoma kurasa za kitabu hicho nje ya msikiti wa Stockholm wakati wa siku kuu ya Waislamu ya Eid al-Adha. Momika, ambaye anajieleza kwenye Facebook kama "mfikiriaji na mwandishi ... mtu asiyeamini kuwa kuna Mungu," alisema maandamano yake yalionyesha hisia zake kuhusu dini hiyo.

Soma pia:Ubalozi wa Sweden mjini Baghdad wachomwa moto

Wiki hii, Momika hakuweza kuchoma kurasa zozote za Quran. Siku ya Alhamisi, akiwa amesimama nje ya Ubalozi wa Irak mjini Stockholm, muandamanaji huyo pekee alikipiga teke kitabu hicho na kuikanyaga bendera ya Irak. Momika pia alifuta miguu yake kwenye picha za kiongozi wa kidini wa Irak Muqtada al-Sadr na kiongozi wa juu wa Iran, Ali Khamenei.

Polisi ya Sweden imekuwa ikitoa ulinzi wakati wa matukio ya uchomaji Qur'an. Hapa ni wakati Momika alipochoma nakala ya kitabu hicho kitakatifu mbele ya Mskiti Mkuu wa Stockholm, Juni 28, 2023.Picha: Caisa Rasmussen/TT NEWS AGENCY/picture alliance

Tukio hilo lilisababisha ghadhabu nchini Irak kabla hata halijatokea. Huko, wafuasi waaminifu kwa kiongozi wa Kishia al-Sadr walivamia ubalozi wa Sweden mjini Baghdad mapema Alhamisi asubuhi na kuuwasha moto.

Kwa nini majibu yalikuwa ya kupita kiasi?

Joto ni kali sana hivi sasa nchini Irak, serikali ya Irak inaongozwa na chama cha kisiasa cha kidini na pia ni mwanzo wa mwezi wa pili mtakatifu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, mshauri wa masuala ya kisiasa wa Irak Jassim Mohamad alisema alipokuwa akielezea ukubwa wa hisia kutoka Irak.

Hasa hii "inamaanisha kuwa hali katika mitaa ya Irak inaelekea kwenye misimamo mikali ya kidini," Mohamad, mkurugenzi wa Kituo cha Ulaya cha Kupambana na Ugaidi na Mafunzo ya Ujasusi, kilichopo katika mji wa Bonn, magharibi mwa Ujerumani, aliiambia DW.

"Inaweza pia kuwa fursa kwa kundi la mhubiri al-Sadr kujitokeza tena kwenye uwanja wa kisiasa na kujiweka katika upinzani dhidi ya serikali ya Irak," aliongeza. Al-Sadr aliachana rasmi na siasa za Iraq mnamo 2022, lakini kiongozi huyo wa kidini bado ana uwezo wa kuitisha idadi kubwa ya waandamanaji mitaani.

"Uamuzi mkali wa serikali ya Iraq wa kumfukuza balozi wa Sweden huenda ulikuja ili kudhibiti kundi la al-Sadr, na pia kwa sababu zake za kiitikadi na kidini," Mohamad alihitimisha.

Historia ya ushari ya mwandamanaji

Katika mitandao ya kijamii, baadhi ya Wairaq walitilia shaka busara ya hatua ya majibu makali ya serikali ya Irak. Wengine walihoji hadharani nia ya Momika na historia yake.

Waandamanaji katika uwanja wa Tahrir mjini Baghdad, wakiwa wamebeba bendera za nchi hiyo na picha za kiongozi wa Kishia Muqtada al-Sadr, Jumamosi Julai 22, 2023, kufuatia ripoti za kuchomwa kwa Qur'an na kundi la mrengo mkali wa kizalendo mbele ya ubalozi wa Irak mjini Copenhagen.Picha: Ali Jabar/AP/picture alliance

Uchunguzi wa kituo cha utangazaji cha France24 ulitazama kwa karibu zaidi machapisho ya mitandao ya kijamii yaliyotolewa na Wairaki waliodai kumtambua Momika, ambaye asili yake ni jimbo la Ninawa, kaskazini mwa Irak na muumini wa madhehebu ya Kikristo.

Soma pia: Umoja wa Mataifa wajadili chuki dhidi ya Waislamu

Momika aliwasili Uswidi mnamo 2018, na viongozi wa Sweden walithibitisha kwamba alipewa kibali cha kuishi kwa miaka mitatu mnamo 2021.

Watafiti wa France24 walithibitisha idadi ya video zinazomwonyesha Momika akiwa amevalia mavazi ya kijeshi, akishirikiana na wanachama wa makundi mengi ya wanamgambo. Walihitimisha kuwa alikuwa mtu yuleyule aliyeanzisha chama cha kisiasa nchini Irak, cha Syriac Democratic Union Party, mnamo 2014, pamoja na kundi la wanamgambo linalohusiana na chama hicho.

Kundi la wanamgambo la Momika, ambalo, kama mengine mengi wakati huo, awali lilianzishwa kupambana na kundi la itikadi kali la "Dola la kiislamu",  IS, inaonekana baadaye lilihusishwa na aina mbalimbali za makundi mengine nchini Irak.

Hayo ni pamoja na makundi yenye mahusiano na Waislamu wa Kishia wanaounga mkono, na wanasaidiwa na, nchi jirani ya Iran, pamoja na  wanamgambo wa Kikurdi ambao wanaunga mkono ajenda ya watu wasioamini Mungu na wakomunisti.

Waandishi wa habari wa Irak waliandika kwamba Momika aliondoka nchini humo kwa sababu ya mzozo wa kugombania madaraka na kiongozi wa wanamgambo wengine wa Kikristo.

Waandamanaji mjini London, Uingereza, wakibeba juu Qur'an wakati wa maandamano ya kupinga uchomaji Qur'an nchini Sweden, Januari 28, 2023.Picha: Loredana Sangiuliano/SOPA/ZUMA/picture alliance

Momika pia anafikiriwa kumuunga mkono al-Sadar katika hatua moja, na kisha kukubaliana na maandamano ya kuipinga serikali nchini Irak. Mjumbe wa baraza la mji aliambia gazeti la The New Arab kwamba Momika alifanya ulaghai katika mji wake wa nyumbani.

Mwandamanaji huyo wa Iraki pia amekuwa matatani na mamlaka ya Sweden baada ya kumtishia mwenzake kwa kisu, gazeti la Sweden la Expressen liliripoti katika mahojiano na Momika mwezi Juni.

Haya yote yaliwapelekea wachunguzi wa France24 kudokeza kuwa msukumo wa Momika wa maandamano yake ya hivi karibuni unaweza kuwa wa kutiliwa shaka. Ripoti nyingine za awali kwa kugha ya Kiarabu zimetoa mashaka kama hayo.

Soma pia: Uturuki yachukuwa hatua dhidi ya uchomaji Quran barani Ulaya

"[Momika] yuko mashughuli kwenye tovuti nyingi za mitandao ya kijamii, haswa TikTok na Facebook," ripoti ya France24 ilibainisha. "Hata hivyo, akaunti zake zote ziliundwa baada ya kupata hadhi ya mkimbizi nchini Sweden ... Momika amechapisha video kadhaa mtandaoni, mara nyingi zikiwa na majina ya nchi zenye Waislamu wengi kwa Kiarabu kama #hashtag. Hii inafanya ionekane kuwa kuna uwezekano kwamba alikuwa akijaribu kuchochea uenezi mkubwa iwezekanavyo kwa uchoamji wake wa Qur'ani."

Madhumuni ya kutia shaka?

Kibali cha ukaaji Sweden cha Momika kinaisha mnamo Aprili 2024, walibaini, na hivi karibuni zaidi alinyimwa ukaaji wa kudumu, hatua muhimu kuelekea kupata uraia.

Momika anasema yeye ni mwanachama wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia nchini Sweden, Sweden Democrats. Hapo awali aliliambia gazeti la Sweden la Aftonbladet kwamba alijiunga na chama hicho mnamo 2022 na angependa kuwania wadhifa wa serikali kupitia chama hicho.

Mwandamanaji Salwan Momika akiinua juu bendera ya Sweden wakati wa maandamano nje ya ubalozi wa irak mjini Stockholm, Sweden, Julai 20, 2023. Momika anatafuta kibali cha ukaaji wa kudumu Sweden.Picha: OSCAR OLSSON/TT News Agency/AFP/Getty Images

Idara ya mahusiano ya umma ya chama hicho cha siasa iliiambia DW kwamba haiwezi kuthibitisha au kukanusha uanachama wa Momika "kwa sababu za faragha na usiri."

Soma pia: UN yaridhia azimio la kupinga chuki za kidini duniani

"Kuhusu madai ya mtu huyu kutaka kugombea wadhifa kupitia chama chetu, hatufahamu juu ya ombi lolote kama hilo hadi sasa na hatuna nia ya kukisia juu ya hali kama hiyo itahusisha nini," ofisi ya habari ya Sweden Democrats iliandika katika taarifa iliyotumwa kwa barua pepe.

Momika mwenyewe hakujibu ombi la mahojiano la DW.

Nini kifuatacho kwa Momika?

Irak yenyewe inataka Momika arejeshwe kutoka Sweden ili aweze kukabiliwa na kesi chini ya sheria za Irak. Tofauti na Sweden, Iraq ina sheria ya kukufuru, ambapo adhabu inaweza kuwa kifungo cha hadi miaka mitatu jela.

Wairan wakiandamana kupinga uchomaji wa Qur'an.Picha: Vahid Salemi/AP/picture alliance

Mwishoni mwa Juni, polisi ya Sweden ilifungua mashtaka ya awali dhidi ya Momika kwa kuchochea chuki na kukiuka marufuku ya moto. Ingawa Sweden haina sheria ya kukufuru na hata inaruhusu maandamano ambayo yanahusisha kunajisi vitu vya kidini, sheria ya matamshi ya chuki nchini humo inakataza uchochezi dhidi ya makundi ya watu kwa misingi ya rangi, kabila, dini, mwelekeo wa kingono au utambulisho wa kijinsia.

Ukweli kwamba Momika alichoma Quran nje ya msikiti unaweza kueleweka kama uchochezi dhidi ya kundi, ilisema polisi ya Sweden. Ikiwa kesi itakwenda mbali zaidi itategemea muafaka wa waendesha mashtaka wa ndani.

Lakini jambo moja ni la uhakika: Hivi sasa amekuwa mtu mashuhuri ulimwenguni pote, maisha ya Momika hayatakuwa rahisi. Tayari ametishiwa kuuawa na kutukanwa mara nyingi. Hapo awali, Momika aliishi katika mji mdogo nje ya Stockholm, lakini video zake nyingi za hivi karibuni zimemuonyesha katika kile kinachoonekana kuwa chumba cha hoteli. Siku ya Ijumaa, vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba alikuwa akihifadhiwa "mahali pa siri" na kwamba hakujutia chochote.

Katika video iliyochapishwa siku ya Alhamisi na mwanasiasa wa Irak, muuza duka mmoja nchini Sweden alikataa kumhudumia muandamanaji huyo aliyechoma Quran.

"Mimi ni Mkristo kutoka Irak na sikubaliani na tabia yako chafu," muuza duka alimfokea Momika. "Umevuka mipaka dhidi ya Uislamu na kumdhuru kila mtu, tukiwemo sisi Wakristo."

Momika anaonekana kuwa ndiye aliyetengeneza video hiyo mwenyewe.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW