Mubarak ashindwa kuwapoza waandamanaji
2 Februari 2011"Hosni Mubarak huyu anayezungumza nanyi leo, ana fahari ya kuitumikia Misri na watu wake kwa miaka mingi ya uhai wake. Nchi hii tukufu ni nchi yangu kama ilivyo kwa Wamisri wengine. Hapa ndipo nilipozaliwa, nikapapigania, nikapalinda utukufu wake na ni hapa ndipo nitakapokufia. Na historia itanihukumu mimi na wengine kwa mema na mapungufu yetu." - Sehemu ya hotuba ya Rais Hosni Mubarak kwa taifa, usiku wa tarehe 1 Februari 2011.
Hapana shaka, mwandishi wa hotuba hii ya Rais Hosni Mubarak, alijitahidi kuchagua maneno yanayogusa hisia za jamii ya Kiarabu ya Misri, ambako mapenzi kwa nchi, heshima, utukufu na ushujaa ni mambo ambayo hayawezi kupimwa kwa chochote.
Lakini nzito kama ilivyokuwa, hotuba hii haikuweza kuzilainisha nyoyo za waandamanaji, waliokusanyika katika miji kadhaa ya nchi hiyo, katika kile kinachoitwa maandamano ya watu milioni moja, ambao hata hajamaliza hotuba yake, walianza kumshambulia: "Irhaal, Irahaal", neno la Kiarabu lenye maana ya "ondoka!"
Hasira zapanda zaidi
Kubwa zaidi ya yote, hasira za waandamanaji zimetokana na kauli yake kwamba, hataondoka madarakani licha ya shinikizo lao, japokuwa ameahidi kuwa hatagombea tena kipindi chengine cha urais, baada ya muhula wake kumalizika Septemba mwaka huu.
Mubarak, mweye historia ya kuwa kamanda wa jeshi la anga, ameondosha kabisa uwezekano wa kumalizia hatima yake kama mwenzake wa Tunisia, Zein El-Abidine Ben Ali, ambaye hivi sasa anaishi uhamishoni nchini Saudi Arabia, baada ya kutangatanga na ndege yake kwenye ya Mediterenian akitafuta nchi ya kutua.
'Mipasho' baina ya Mubarak na waandamanaji
Sasa ameamua kuitisha kile, wanachokiona wachambuzi wa mambo, kama ushindani wa maneno ya vijembe baina yake na waandamanaji. Alipoapa kufia Misri, wao wameapa kufia kwenye uwanja wa maandamano.
Alipowakumbusha namna alivyoitumikia nchi yake kwa utiifu, na utayarifu wake wa kuondoka na heshima, walimkumbusha namna walivyomuheshimu na kumuogopa, lakini naye akawasaliti kwa kuwakandamiza na wakamuonesha utayarifu wao wa kuhimili chochote chengine, alimradi tu ang'oke.
Mwandamanaji mmoja wa kike, alifikia umbali wa kusema kwamba ni ama za Wamisri ama za Mubarak, lakini mmoja lazima ashindwe kati yao.
"Sisi tunabakia hapa hapa mpaka Hosni Mubarak aende zake Jedda, au Tel Aviv. Kama anaapa kufa kwenye ardhi ya Misri, sisi tunaapa kufa kwenye uwanja huu wa Tahrir." Álisema mwandamanaji huyo.
Mubarak yuko mbali na watu wake
Kwa vyovyote vile, kupitia hotuba hii, Mubarak amejichorea taswira yake ya kuwa kiongozi mkongwe anayeishi kwenye dunia yake mwenyewe, bila ya kuhisi kile wanachokihisi raia wake.
Fahari, gambo na heshima aliyoizungumzia kupitia historia yake, haiwahusu kabisa vijana wanaondamana, ambao wengi wao wameishi ndani ya miaka 30 ya utawala wake na sio kabla ya hapo.
Vijana hawa hawakujua utawala mwengine usipokuwa wake, na kwao Mubarak si mwanajeshi shujaa kwenye jeshi la anga, bali ni kiongozi aliyechangia kufeli kwao kimaisha, jambo ambalo hawawezi kumsamehe wala kumvumilia tena.
Hata hivyo, ni wazi kuwa Mubarak ameshaamua kubakia madarakani hadi dakika ya mwisho, na hakuna kinachoweza kumbadilisha mawazo yake kwa muda huu uliobakia.
Jeshi lataka Wamisri warudi majumbani
Wakati huo jeshi nchini Misri limetoa taarifa ya kuwaomba waandamanaji kurudi nyumbani na kuendelea na shughuli zao za maisha, huku likisambaza ujumbe mfupi wa simu za mkononi unaowaomba raia kulinda nchi, mali na heshima ya taifa.
Ujumbe mmoja uliokusudiwa vijana umesomeka: "Vijana wa Kimisri, tahadhari na uvumi, sikiliza na fikiria kwa makini. Misri inakuhitaji sana. Ilinde."
Hadi sasa, maandamano haya yanayoingia siku yake ya nane leo, yameshagharimu roho 300 za Wamisri, wengi wao wakiwa raia, huku wengine 3000 wakijeruhiwa. Huduma za kijamii na kiuchumi zimesimama katika maeneo mengi ya nchi hiyo, huku wawekezaji wakiondoa mitaji yao katika taasisi za kifedha.
Na bado si wazi, gharama gani nyengine itatosha kuleta mabadiliko wanayoyadai waandamanaji!
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFPE
Mhariri: Othman Miraj