Muda wa kupiga kura waongezwa Misri
28 Mei 2014Hata baada ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa tena hii leo asubuhi nchini Misri bado wapiga kura hawakujitokeza kwa wingi hali inayoashiria kuwa uchaguzi, haujatiliwa maanani nchini humo.
Hata hivyo kujitokeza kwa wingi kwa wapiga kura katika uchaguzi huu ina maana kubwa kwa mkuu wa zamani wa majeshi Abdel-Fattah el-Sissi, anayetarajia hali hiyo kuwa ushahidi wa uhalali wa kumuondoa rais Mohammed Mursi madarakani mwezi Julai mwaka jana.
Morsi ni rais wa kwanza nchini Misri aliyechaguliwa kihalali, chama chake cha Udugu wa Kiislamu kimeususia uchaguzi huo.
Aidha wapinzani wanasema idadi ndogo ya wapiga kura inaonesha raia wa Misri hawamuungi mkono jenerali huyo wa zamani na sio tu kwa maadui wake wa chama cha Morsi cha Udugu wa Kiislamu bali pia miongoni mwa raia wengi nchini humo wanaosema Al Sisi hana suluhu kwa matatizo yao huku wakihofia Misri itatawaliwa tena kama ilivyokuwa wakati wa rais wa zamani wa Misri, Hosni Mubarak.
Hii leo asubuhi mgombea wa urais, Hamdeen Sabahy, aliwaondoa wajumbe wake wote katika vituo vya kupigia kura akipinga uamuzi wa tume ya uchaguzi wa kuongeza muda wa kupiga kura.
Idadi ya waliopiga kura ni ndogo mno, yasema tume ya uchaguzi
Tume ya uchaguzi ilitangaza kuongeza muda huo saa chache kabla ya vituo vya kupigia kura kufungwa siku ya Jumanne. Hii imetokana na takriban asilimia 37 ya watu waliojitokeza kupiga kura katika siku mbili zilizotengewa zoezi hilo, idadi inayosemekana kuwa ndogo mno.
Katika kituo kimoja cha kupigia kura wilayani Shubra kilichosajili takriban wapiga kura 6,200, kililuwa kitupu muda mfupi baada ya kufunguliwa hii leo asubuhi. Walioripotiwa kuwa ndani ya kituo hicho ni maafisa wa kupiga kura, wanajeshi pamoja na polisi.
Abdel-Fattah el-Sissi, Mkuu wa idara ya ujasusi wakati wa utwala wa rais wa zamani Hosni Mubarak anatarajiwa kushinda katika uchaguzi huu ambapo wafuasi wake wanamuona kama mtu anayeweza kumaliza msukosuko wa kisiasa ulioikumba Misri kwa zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Takriban asilimia 52 ya wapiga kura walipiga kura mwaka wa 2012 ambapo rais aliyepinduliwa madarakani na jeshi lililoongozwa na jenerali wa zamani Abelfattah Al Sisi, Mohammed Mursi, alishinda uchaguzi huo.
Matokeo ya uchaguzi nchini Misri yanatarajiwa kutangazwa Alhamisi ijayo.
Mwandishi: Amina Abubakar/AP/dpa/Reuters
Mhariri Josephat Charo