Muda wa M23 kusalimisha silaha wakamilika bila matunda
25 Septemba 2023Wakati huohuo, mashirika ya kiraia huko mkoani kivu kaskazini yameongeza shinikizo dhidi ya serikali ya Kongo ,yakiitaka kuyakomboa maeneo yote yanayokaliwa na waasi wa M23.
Mwito huo wa asasi za kiraia umekuja baada ya vikosi vya jeshi la Kongo,FARDC kuchukua udhibiti wa mji wa kimkakati wa Mushaki ambao uliachwa na waasi wa M23.
Serikali ya Kongo kupitia naibu waziri wa mambo ya nje, Christophe Lutundula ilitowa ma saa 72 kwa waasi wa M23 kuweka silaha chini kuanzia ijumaa hadi jana jumapili lakini kundi hilo limeendelea kuzishikilia ngome zao.
Kongo yaomba jumuiya kimataifa kuwawekea vikwazo wahusika wa uvamizi wa Rwanda nchini humo
Kauli ya naibu waziri Lutundula ilifuatia ile ya Rais Felix Tshisekedi mjini NewYork wiki iliopita kwamba serikali haitofanya mazungumzo na waasi wa M23.
Wiki iliyopita, waasi haao wa M23 walionekana kwenye mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali wilayani Rutshuru na Nyiragongo wakiwashawishi wananchi kuwaunga mkono kwa kile wanacho taja kuwa njia yakutafuta amani na kuonesha utayari wao wakupigana dhidi ya serikali .
Wakati huohuo, vikosi vya jeshi la congo, FARDC vilidhibiti tena mji wa mushaki umbali wa kilomita 40 na mji wa Goma ,ambako vyombo vya usalama vimefaulu kuifungua barabara hiyo muhimu.
Huo ni mji wa kwanza kuchukuliwa na FARDC katika eneo ambalo jeshi la kikanda kutoka nchini Burundi lilitumwa kuulinda mji huo tangu novemba mwaka uliopita.
Marekani yawawekea vikwazo maafisa wa Rwanda na Kongo
Akiutembelea mji huo mwishoni mwa wiki iliyopita, Peter Cirimwami gavana wa muda na kamanda wa operesheni za kijeshi mkoani kivu kaskazini amewataka raia kuunga mkono juhudi zakutafuta amani eneo hilo.
Kando na kuitaka serikali ya congo kuvunja ukimya wake kwa kulitokomeza kundi hilo la waasi, mashirika ya kiraia eneo hilo yameomba kurudishwa kwa mamlaka za serikali katika maeneo yanayodhibitwa na M23.
Tangu Februari mwaka huu,waasi wa M23 wanaotuhumiwa na serikali mjini kinshasa kupata usaidizi wa Rwanda waliuteka mji huo wa mushaki ambapo waliweka sheria zao nakuwalipisha kodi kwa nguvu wafanyakazi wa eneo hilo.
Haya yamejiri miezi michache kabla ya raia wa congo kushiriki uchaguzi mkuu tarehe 20 desemba huku mamia ya wengine wakiwa bado ndani ya makambi ya wakimbizi