Uchaguzi Nigeria waendelea baada ya matatizo ya teknolojia
29 Machi 2015Rais Goodluck Jonathan --ambaye anapambana na kiongozi wa zamani wa kijeshi Mohammad Buhari --pamoja na takriban magavana watatu kutoka chama chake tawala ni miongoni mwa wale ambao taarifa zao za "biometriki" hazikuweza kusomwa na vifaa, ambavyo vimekusudiwa kupambana na udanganyifu. Badala yake walilazimika kuchukuliwa taarifa zao kwa mkono.
Chama cha Jonathan cha Peoples Democratic Party PDP kimeiita hali hiyo "aibu kubwa ya kitaifa na kwamba ni uthibitisho wa msimamo wao dhidi ya teknolojia hiyo.
"Walipaswa kufanya majaribio katika chaguzi ndogo kabla ya kuutumia kwa ajili ya uchaguzi mkubwa kama huu," amesema msemaji wa kampeni ya rais Jonathan Femi Fani-Kayode.
Buhari, mpinzani mkuu wa Jonathan katika uchaguzi huu ambaye chama chake cha All Progressives Congress APC kimeunga mkono vifaa hivyo vya kusoma taarifa za kadi za wapiga kura , hata hivyo , amedokeza kwamba mzozo huo umetengenezwa kuwa mkubwa bila sababu.
"Haya yote, nadhani , ni fikira potofu kuhusu uchaguzi nchini Nigeria ambazo hazina ulazima kwasababu ya matatizo katika jumla ya majimbo matano tu, " amesema.
Urefushaji wa uchaguzi huo kwa muda wa masaa 24 ni kitu cha kawaida, "amesema", na kuongeza baada ya kupiga kura katika jimbo anakotoka la Katsina , katika upande wa kaskazini wenye Waislamu wengi.
Mtafaruku kuhusiana na kushindwa kufanyakazi kwa teknolojia kumeongeza katika matatizo ya upigaji kura katika taifa hilo lenye wakaazi wengi barani Afrika ambapo ni pamoja na maafisa kuwasili wakiwa wamechelewa-- ama katika wakati mwingine hawakuwasili kabisa.
Boko Haram lashambulia
Kundi la Boko Haram , ambalo limekuwa likipata kutajwa sana wakati wa kampeni, pia limechukua nafasi kubwa, na kutimiza ahadi yake ya kuchafua kile inachoona kuwa uchaguzi ni "kinyume na Uislamu" kwa kufanya mashambulio kadhaa.
Siku ya Ijumaa (27.03.2015), kiasi ya watu 23 walichinjwa na majumba kutiwa moto mjini Buratai, kiasi ya kilometa 200 kutoka katika mji mkuu wa jimbo la Borno, licha ya kwamba haijawa wazi iwapo ghasia hizo zilihusiana na uchaguzi.
Siku ya Jumamosi (28.03.2015) kiasi ya watu saba wameuwawa katika wimbi la mashambulizi ya risasi ambayo watu walioshuhudia wanalilaumu kundi hilo la Waislamu katika jimbo la kaskazini mashariki la Gombe.
Matatu kati ya mashambulizi hayo yalifanyika dhidi ya vituo vya kupigia kura.
Afisa wa tume ya uchaguzi katika wilaya ya Nafada , ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe, amesema watu waliokuwa na silaha walisikika wakipiga kelele: "Hatukuwapa tahadhari juu ya kutoshiriki uchaguzi?"
Kundi hilo la Waislamu limekuwa mara kwa mara likishambulia mji wa Nafada, lakini chama cha APC siku ya Jumamosi kiliwalaumu wapinzani wao wa kisiasa .
Leo Jumapili (29.03.2015) kutakuwa pia na ulinzi mkali wakati uchaguzi utakapokuwa unaendelea, kutokana na historia ya zamani ya Nigeria kuhusiana na ghasia zinazoambatana na uchaguzi ambapo mwaka 2011 watu 1,000 waliuwawa baada ya matokeo kutangazwa.
Huenda uchaguzi ukarefushwa zaidi
Tume huru ya taifa ya uchaguzi imesema matokeo jumla yatatangazwa katika muda wa masaa 48 baada ya kufungwa vituo vya uchaguzi. Lakini hali hiyo ya lazima ya uchelewesho , ambayo itashuhudia wale walioathirika na matatizo ya teknolojia kuandikishwa kwa mkono, huenda watarefusha muda wa mwisho ambao tayari umelegezwa.
Mwenyekiti wa tume huru ya taifa ya uchaguzi Attahiru Jega amekiambia kituo cha televisheni ya taifa NTA katika mahojiano jana Jumamosi(28.03.2015) kwamba kile kilichotokea kwa Jonathan "kinasikitisha na aibu kwa taifa".
Lakini ameongeza kwamba "kwa jumla" tunaamini kwamba mbali na changamoto hizo mambo yalikwenda vizuri sana" na kwamba watu wengi walijitokeza kupiga kura.
Msemaji wa tume hiyo Kayode Idowu amesema upigaji kura utafanyika leo Jumapili (29.03.2015)katika vituo 300 vya uchaguzi kutoka jumla ya kiasi ya vituo 150,000 nchi nzima.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Idd Ssessanga