1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mueller asema, ripoti yake haikumuondolea Rais Trump hatia

30 Mei 2019

Robert Mueller ambaye alikuwa mchunguzi maalum kuhusu iwapo Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani asema, ripoti yake haikumuondolea rais hatia lakini pia kumshitaki rais kwa uhalifu halikuwa suala la kuzingatiwa."

USA PK vom US-Sonderermittler Robert Mueller in Washington
Picha: Reuters/J. Bourg

Mchunguzi maalum kuhusu uingiliaji wa Urusi katika uchaguzi mkuu wa Marekani mwaka 2016 Robert Mueller, amesema uchunguzi wake uliodumu kwa miaka miwili haukumuondolea hatia rais Trump, bali hakuwa na mamlaka ya kumfungulia mashtaka rais aliyeko madarakani.

Akitoa hotuba ya kwanza kuhusu uchunguzi wake juu ya iwapo Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani mwaka 2016 ama la, mchunguzi huyo maalum Robert Mueller amesema asingeweza kusema kuwa Rais Donald Trump hakuwa na hatia, baada ya kuorodhesha visa kama 10 vya Rais Trump kujaribu kuzuia uchunguzi.

Rais aliyeko madarakani hawezi kushtakiwa

Siku ya Jumatano, Mueller alieleza kuwa alizuiliwa na sera ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu katika wizara ya sheria zinazosema kuwa rais aliyeko madarakani kamwe hawezi kushtakiwa kwa kosa la jinai, hata kama kuna ushahidi thabiti kiasi gani. Mueller aliongeza kuwa lau wangekuwa na uthibitisho wazi kuwa rais hakuwa na hatia, wangesema hayo.

"Ofisi ya mchunguzi maalum ni sehemu ya wizara ya sheria na kulingana na kanuni, inaongozwa na sera za wizara. Kwa hivyo kumshitaki rais kwa uhalifu halikuwa suala la kuzingatiwa"

Rais trump anashikilia kuwa uchunguzi wa Mueller ulimuondolea lawama na hakuna ushahidi dhidi yake uliopatikana kuhusu tuhuma zinazomuandama.Picha: Reuters/L. Millis

Mueller amesema kesi hiyo sasa iko mikononi mwa bunge. Kauli yake tayari imeibua miito mipya kutoka kwa wabunge wa chama cha Democrat wanaotaka mchakato wa kumuondoa rais madarakani uanze.

Lakini Rais Trump ambaye amekuwa akiutaja uchunguzi huo kuwa njama ya kisiasa dhidi yake na porojo tu, amesema kesi hiyo imeshafungwa.

Miito ya Trump aondolewe yaanza

Muda mfupi baada ya Mueller kumaliza kuzungumza, Trump aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, "hakuna kinachobadilika kwenye ripoti ya Mueller. Hakukuwa na ushahidi wa kutosha na kwa hivyo, katika hali kama hiyo mtu hana hatia nchini mwetu. Kesi imefungwa! Asante" mwisho wa kunukuu.

Seneta wa chama cha Democrat Elizabeth Warren aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa, Mueller hajaacha shaka lolote. Katiba sasa inaliachia bunge kuchukua hatua ya kumuondoa madarakani Trump.

Kauli za Mueller ambazo amezitoa mwezi mmoja baada ya kutoa ripoti yake ya uchunguzi kuhusu juhudi za Urusi kumsaidia Trump kumshinda aliyekuwa mshindani wake Hillary Clinton, zimeonekana kulenga kuthibitisha uhalali wa uchunguzi wake dhidi ya malalamiko ya rais, na pia kueleza uamuzi wake wa kutofikia jibu kamili ikiwa Rais Trump alijaribu kuzuia haki kwenye uchunguzi huo.

Ripoti hiyo ilibaini kuwa hakukuwa na ushirikiano kati ya timu ya kampeni ya Trump na Urusi kwenye uchaguzi wa Marekani mwaka 2016.

Vyanzo: AFPE, APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW