Mugabe achangia Umoja wa Afrika dola milioni moja
4 Julai 2017Kwa miaka kadhaa sasa karibu asilimia 60 ya bajeti ya matumizi ya Umoja wa Afrika imekuwa ikifadhiliwa na wafadhili ikiwa ni pamoja na Umoja wa Ulaya, Benki ya Dunia na mataifa mengine tajiri nje ya bara hilo.
Rais Robert Mugabe ambaye yuko madarakani tangu Zimbabwe ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1980, amesema kutegemea msaada kutoka kwa wafadhili kunasababisha mataifa makubwa kuingilia masuala ya ndani ya Umoja wa Afrika.
Rais Mugabe ambaye kwasasa ana umri wa miaka 93 amesema alilazimika kuuza mifugo yake 300 mwezi Mei ili kutimiza ahadi ya miaka miwili iliyopita.
Akikaririwa na televisheni ya taifa ya Zimbabwe Rais Mugabe amesema Afrika inapaswa kufadhili mipango yake wenyewe na kuwa taasisi kama ya AU haipaswi kutegemea pekee misaada kutoka kwa wafadhili.
Bajeti ya Umoja wa Afrika kwa mwaka wa 2017 ni Dola milioni 782 ikipanda kutoka Dola milioni 416 mwaka jana. Viongozi wa Umoja huo mwaka jana walikubaliana kimsingi kutoza asilimia 0.2 katika mauzo ya nje ya bidhaa kutoka barani humo ili kufadhili shughuli za Umoja huo.
Zimbabwe ambayo uchumi wake uliathiriwa na ukame uliolikumba taifa hilo mwaka jana haijaweka bayana mchango wake kwenye Umoja wa Afrika.
Mataifa matano barani humo yanayo ongoza kuchangia kwenye Umoja wa Afrika ni Algeria, Misri, Libya, Nigeria na Afrika Kusini.
AU yatakiwa kuzisaidia nchi zinazokabiliwa na njaa
Wakati huohuo Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahmat hapo jana amezikusoa nchi wanachama wa Umoja huo kwa kushindwa kuonesha mshikamano kwa nchi zinazokabiliwa na janga la njaa barani humo.
Faki ambaye alikuwa waziri wa mambo ya nchi za nje wa Chad kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwezi Januari amesema hawezi kuficha hisia zake kuhusiana na jinsi anavyoguswa na hali ya ukimya uliopo kutokana na mataifa ya Afrika kushindwa kuchukua hatua katika kuzisaidia nchi zinazo kabiliwa na njaa barani humo.
Kuchaguliwa kwa Faki kulikuja siku kadhaa baada ya Umoja wa Mataifa kusema ulimwengu unakabiliwa na mgogoro mkubwa wa kibinadamu tangu kumalizika kwa vita ya pili ya dunia huku kiasi ya watu milioni 20 wakikabiliwa na utapia mlo pamoja na njaa nchini Yemen, Somalia, Sudan Kusini na Nigeria.
Mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika safari hii umejikita katika ajenda ya jinsi gani ya kuweza kufanya mageuzi ndani ya umoja huo pamoja na kuuwezesha kuto tegemea ufadhili kutoka nje.
Wakati huohuo Djibouti itautaka Umoja wa Afrika kusaidia katika kutatua mgogoro wa muda mrefu wa mpaka kati yake na Eritrea hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa taifa hilo la pembe ya Afrika Mohamoud Ali Youssouf alipozungumza na shirika la habari la AFP.
Vikosi vya jeshi la Qatari ambavyo vilikuwa vinaweka doria katika mpaka wa nchi hizo mbili viliodolewa mwezi uliopita baada ya Djibouti na Eritrea kuungana na Saudi Arabia wakati nchi hiyo ilipovunja uhusiano na Qatari kuhusiana na madai ya Qatari kuunga mkono makundi ya kiisilamu yenye itikadi kali.
Mwandishi: Isaac Gamba/ AFPE
Mhariri :Yusuf Saumu