Mugabe asema ICC haina nafasi Afrika.
16 Juni 2015Baada ya rais wa Sudan kulikwepa agizo la mahakama hiyo iliyoamuru akamatwe,wakati akihudhuria mkutano wa viongozi wa bara la Afrika uliomalizika jana nchini Afrika Kusini :Rais huyo wa Sudan hatimae aliondoka na kurudi nyumbani .
Shirika la Habari la Africa, lenye makao yake nchini Afrika Kusini, lilimnukuu Mugabe akisema wakati wa kufunga mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika mjini Johannesburg jana usiku kwamba Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu haitakiwi barani Afrika.
Mugabe alisema,"hapa si makao makuu ya ICC. Hatuitaka katika kanda hii kabisa." Mugabe ambaye ni Mwenyeiki wa mwaka huu wa Umoja wa Afrika, wadhifa unaozunguka miongoni mwa viongozi wa Umoja huo alisema mkataba uliounda hakutiwa saini na Umoja wa Afrika bali nchi moja moja, akiongeza kuna fikra ya kujitoa katika mahakama hiyo.
Afrika Kusini imesaini waraka unaounda mahakama hiyo ya kimataifa, lakini baadhi ya viongozi wakiafrika wanasema mahakama hiyo inawaandama tu viongozi wakee wa kiafrika na Umoja wa Afrika umesema wajumbe katika mkutano huo wa kilele wa Johannesburg wana kinga ya kibalozi.
Shirika la habari la Africa lilioripoti kwamba, kwa mujibu wa Rais Mugabe, Rais jacob Zuma wa Afrika kusini alisema hatoiruhusu polisi kumkamata Rais Bashir. Msema wa ofisi ya Zuma alitaka maswali yote aulizwe msemaji wa serikali bibi Phumla Williams ambaye hakuweza kupatika hii leo kwa kuwa ni siku ya mapumziko ya kitaifa nchini humo.
Mjini The Hague, naibu mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo ya uhalifu ya kimataifa James Stewart alisema Afrika Kusini ilikuwa na jukumu kisheria kumkamata Rais Bashir ili afikishwe mahakamani mbele ya mahakama hiyo.
Kiongozi wa Sudan aliyewasili Khartoum jana anasakwa na mahakama hiyo ya ICC kujibu mashtaka ya kuhusika na uhalifu wa kivita, unaohusishwa na mgogoro wa jimbo la magharibi mwa Sudan la Darfur.
Mwanasheria Nickl Kaufman anayewawakilisha wahanga kadhaa katika kesi ya darfur kwenye mahakama ya ICC, leo aliwasilina na mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo, akiwataka majaji kuwasilisha hati rasmi ya malalamiko kwa serikali ya Afrika Kusini kutokana na kushindwa kutii amri ya mahakama hiyo na kumkamata Bashir na kutaka pia suala hilo liwasilishwe mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo, Marekani imeelezea kusikitishwa kwake kutokana na rais Bashir kuhudhuria mkutano huo wa viongozi wa Umoja wa Afrika na kushindwa kwa Afrika Kusini kumtia nguvuni. Marekani yenyewe si mwanachama wa ICC ,ikiwa imekataa kusaini waraka uliounda mahakama hiyo.
Mwandishi: Salma Mkalibala,AP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman.