1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mugabe auwekea kiwingu mkutano wa Afrika na Ulaya

7 Desemba 2007

LISBON

Viongozi wa Afrika na Ulaya wako mjini Lisbon Ureno kwa mkutano wa kilele unaokusudia kuanzisha uhusiano mpya lakini uko hatarini kutiwa kiwingu na kuhudhuria kwa Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe.

Mkutano huo wa siku mbili katika mji mkuu wa Ureno ambao ni wa kwanza kufanyika baada ya kipindi cha miaka saba unatazamiwa kudhibitiwa na masuala kama vile biashara,uhamiaji, mazingira na haki za binaadamu wakati utakapoanza rasmi hapo kesho asubuhi.

Rais wa bunge la Ulaya Hans-Gert Pöttering anasisitiza kwamba uhusiano kati ya Afrika na Umoja wa Ulaya ni muhimu zaidi kuliko yote.

Hata hivyo kuwepo kwa Mugabe katika tafrija ya chakula cha jioni leo hii na kususiwa kwa mkutano huo na Waziri Mkuu wa Uingereza Gordon Brown ni ukumbusho wa jinsi uhusiano ulivyo mgumu kati ya Ulaya na makoloni yake ya zamani.

Mugabe ambaye kwa kawaida amepigwa marufuku katika nchi za Umoja wa Ulaya kutokana na kuhujumu uchaguzi wa kuchaguliwa tena mwaka 2002 amewasili Lisbon jana usiku baada ya kupata mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo licha ya juhudi kubwa za Brown kutaka azuiliwe kushiriki mkutano huo.