1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMyanmar

China yairai Myanmar kurejesha utulivu

6 Novemba 2023

China imeitolea wito Myanmar kushirikiana ili kuhakikisha wanarejesha utulivu katika mpaka kati yao. China imetoa wito huu wakati naibu waziri wa mambo ya nje wa China Nong Rong alipofanya ziara nchini Myanmar.

Myanmar | Militär
Jeshi la Myanmar limeahidi kulipiza kisasi dhidi ya mashambulizi ya wanamgambo kaskazini mwa taifa hilo.Picha: AFP/Getty Images

Nong akiwa ziarani kati ya Novemba 3 hadi 5 nchini Myanmar amesema China ina matumaini kwamba Myanmar utarejesha hali ya utulivu na kuahidi kusaidia pande zote kushughulikia vizuri tofauti baina yao na kuwapatanisha kupitia mazungumzo haraka iwezekanavyo. Nong pia ameiomba Myanmar kuchukua hatua za kuimarisha usalama wa watumishi raia wa China pamoja na taasisi zake zilizopo nchini humo.

Tovuti ya habari ya Asia Times imeripoti kwamba raia mmoja wa China aliuawa na baadhi yao kujeruhiwa siku ya Jumamosi baada ya bomu lililorushwa na Myanmar kupotea na kuangukia kwenye eneo la mpaka wa China.

Myanmar imekuwa katika machafuko tangu utawala wa kijeshi ulipochukua mamlaka baada ya mapinduzi ya Februari 2021 yaliyoondoa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia iliyoongozwa na mshindi wa Tuzo ya Kimataifa ya Amani ya Nobel, Aung San Suu Kyi.

Makundi ya waasi yanayounga mkono demokrasia katika baadhi ya maeneo yameungana na makundi ya kikabila ya wapiganaji wa msituni ambayo yamekuwa yakifanya kampeni kwa miongo kadhaa ya uhuru zaidi katika kukabiliana na vikosi vya utawala wa kijeshi.

Soma piaViongozi wa ASEAN walitaka jeshi la Myanmar kuacha kuwashambulia raia

Mkuu wa utawala huo wa kijeshi amesema mapema leo kwamba watalipizia kisasi mashambulizi yanayofanywa na makundi hayo kaskazini mwa nchi, huku wakikamata miji na kuzifunga barabara muhimu za kibiashara hadi China, hii ikiwa ni kulingana na msemaji wa utawala huo Zaw Min Tun, aliyenukuliwa na vyombo vya habari vya serikali.

Wanamgambo wa kundi la Kachin Independence Army wakitembea kwenye pori kaskazini mwa Myanmar. Makundi ya wanamgambo yanakabiliana na kile wanachoita utawala wa kidiktetaPicha: Esther Htusan/AP Photo/picture alliance

"Makundi ya kikabila ya wapiganaji yamekuwa yakiendeleza propaganda kwa kusema yamekamata majiji yote ya jimbo la kaskazini la Shah. Pia kuna propaganda za taarifa potofu zinazosambaa juu ya mahali na namna makundi hayo yaliyojihami kwa silaha yanavyofanya mashambulizi," amesema Zaw Min Tun.

Taarifa ya pamoja ya makundi matatu wanamgambo hao yanayojiita "muungano wa makundi ya udugu" imesema mashambulizi hayo yamenuia kuuangusha kile walichoita "utawala wa kidikteta" nchini Myanmar pamoja na kuyalenga magenge ya wahalifu yanayoendesha utapeli wa mawasiliano ya simu, ambao kulingana na muungano huo yanalindwa na utawala wa kijeshi.

Wakati serikali za magharibi zikilaani utawala huo wa kijeshi nchini Myanmar na kuiwekea vikwazo, China pamoja na Urusiwamekuwa wakiwaunga mkono majenerali wake. China imesema inaunga mkono namna Myanmar inavyoshughulikia matatizo yake na kuieleza jumuiya ya kimataifa kuheshimu uhuru wa Myanmar.

Soma pia:Vikwazo dhidi ya Myanmar ni chagizo kwa demokrasia

Katika hatua nyingine, Thailand inajaribu kuwarejesha nyumbani raia wake takriban 162 waliokwama kutokana na mapigano nchini Myanmar ambao kwa sasa wako salama katika mji mkuu Yangon. Bado kunafanyika utaratibu wa kuwasaidia raia wengine 60 kwa ushirikiano na jeshi la Myanmar.

Waziri mkuu wa Thailand Srettha Thavisin alisema Alhamisi iliyopita kwamba Wathailand na raia wengine walikuwa ni miongoni mwa watu waliokwama kaskazini mwa Myanmar kufuatia mapigano hayo kwenye jimbo la Shah.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW