1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

MUNICH NA SCHALKE FINALI YA KOMBE LAUJERUMANI- DFB:

21 Aprili 2005

BUNDESLIGA-tukianza na Ligi ya Ujerumani iliorudi uwanjani hivi punde, Bayern Munich iko njiani kutwaa taji kutoka mikono ya mabingwa Werder Bremen na mwishoe kuondoka hata na vikombe vyote 2-kombe la Ligi na la shirikisho la dimba la Ujerumani (DFB POKAL).

Munich kati ya wiki ilikata tiketi yake ya finali ya kombe la Shirikisho kufuatia ushindi wa mabao 2:0 dhidi ya Armenia Bielegfeld kati ya wiki hiki hii.Ilikua nahodha wa timu ya Taifa Michael ballack aliufumania mlango wa Bielefeld katika dakika ya 3 ya mchezo na kutia bao la kwanza la Munich.

Kwa kweli, Bielefeld ikicheza na mshambulizi wao hatari kutoka Afrika Kusini,Delron Buckley, ndio iliotam,ba wakati mwingi uwanjani,lakini muda mfupi kabla ya firimbi ya mwisho,Roy Makkay aliipatia Munich bao la pili kupitia mkwaju wa penalty.Laiti lakini sio kipa wao Oliver Kahn basi changamoto hii ingelimalizika vyengine,kwani aliokoa mara 2 wazi wazi.Timu hizi 2 zilipokutana mara iliopita katika Bundesliga msimu huu, ilikua Bielefeld ilioilaza Bayern munich kwa mabao 3:1.mabao 2 kati ya hayo alitia muafrika Kusini, Delron Buckley.

Juzi lakini alibidi mwishoe kutolewa nje ya uwanja na rifu alipolalamika kupita kiasi na hata kujaribu kumpiga kumbo rifu uwanjani.

Ni chini ya hali hii, timu 18 za Bundesliga zimerudi uwanjani jioni hii kuania pointi 3 nyengine huku yakisalia mapambano 5 kabla msimu kumalizika.

Mwishoni mwa juma lililopita,Bayern Munich iliokua bega kwa bega kitambo kirefu na Schalke 04,iliizaba Hannover 2:1 na kupanua mwanya wa pointi 6 kwavile Stuttgat ilipoteza pointi sawa na Schalke.Schalke ililazwa na Hamburg kwa mabao 2:1.Bao la ushindi lilitiwa na Emile Mpenza .Mpenza akiichezea zamani schalke na ndie aliewatilia Schalke kitumbua chao mchanga msimu huu wasitwae ubingwa.

Zikisalia mechi 5 kabla kufunga msimu na Munich ikiongoza kwa pointi 2,ni vigumu kuwa watateleza na kila ishara zaonesha Bayern Munich waliondokea mikono mitupu msimu uliopita, huu ni msimu wao alao nyumgbani.Wanaongoza wakati huu Ligi kwa pointi 62 kabla kumalizika kwa changamoto za mwishoni mwa wiki hii.

Wiki hii, FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni,lilitoa orodha yake ya timu 20 za dimba duniani .katika orodha hiyo,Jamhuri ya Czech imechupa hadi nafasi ya pili nyuma ya mabingwa wa dunia-Brazil.hii inafuatia ushindi wao mara 2 mwezi uliopita katika kinyan’ganyiro cha kuania nafasi katika finali za mwaka ujao za Kom be la dunia hapa Ujerumani.Ushindi wa Jamhuri ya Czech dhidi ya Finland na Andorra umewaweka wacheki nafasi nzuri katika kanda ya Ulaya –kundi la kwanza kuja katika kombe lijalo la dunia.

Argentina inafuata jamhuri ya Czech nafasi ya tatu na ndio inayoongowakati huu kanda ya Amerika Kusini ya kuania tiketi 5 za Kombe lijalo la dunia .Tangu Holland na hata Uingereza zimepanda nafasi 2 kutoka chini ya orodha hiyo ya FIFA.Holland imeangukia nafasi ya 5 na Uingereza ya 6.Spain na Mexico zimeteremka chini nafasi ya 7 na ya nane. Ujerumani imeangukia nafasi ya mwisho ya 20 licha ya kuwa wao ni mabingwa mara tatu wa dunia.Hii,lakini adai kocha wa timu ya Taifa Jürgen klinsmann haishughulishi Ujerumani.Anadai Ujerumani isijumuishwe kabisa katika orodha hiyo wakati huu kwavile haishiriki katika kinyan ‘ganyiro cha kuania za finali ya Kombe la Dunia.Ujerumani kama mwenyeji itaingia bila kupingwa.

Mchango wa FIFA kugharimia ujenzi mpya wa viwanja na zana za dimba katika nchi za Asia zilizoathiriwa na msiba wa Tsunami mwishoni mwa mwaka jana umefikia Euro milioni 8.3.Katika kitita cha Euro milioni 5.8 kilichotolewa,Indonesia na Sri Lanka, kila moja imejipatia Euro milioni 1.9 wakati india na Maldives kila moja imepata Euro 765,000.Thiland imepewa Euro 383 na Bangladesh Euro 76,000.

Bw.Mohammed Bin Hammam,rais wa shirikisho la dimba la Asia ambae pia ni mjumbe wa Halmashauri-tendaji ya FIFA amesema kwamba fedha hizo zitatumika kukarabati viwanja vya mpira vilivoteketezwa na Tsunami.

MBIO ZA MARATHON:

Waandazi wa mbio za marathon za miji mikuu 5 wanapanga kuanzisha mfumo wa mashindano ya Grand Slam kwa kuweka kitita maalumu cha mshindi atakaibuka bingwa wa mashindano ya marathon ya jiji la london,New York ,Boston ,Chicago na Berlin.

Duru zimearifu kwamba, wakurugenzi wa mbio za marathon kutoka miji hiyo 5 walikutana huko St.Etienne,Ufaransa mwezi uliopita wakati wa mashindano ya ubingwa wa nyika ulimwenguni-world cross-country championship kushauriana juu ya jinsi gani wangefanya kazi pamoja.

Wakatangaza kwamba, shauri la mashindano makuu ya GRAND SLAM kwa mbio za marathon yamkinika likaibuka wakati wa mashindano ya ubingwa wa riadha wa dunia yaliopangwa Helsinki,August mwaka huu.

Mkurugenzi wa NEW YORK MARATHON Mary Wittenberg amearifu kwamba wakurugenzi wote wa mbio kutoka miji hiyo wanwasiliana mara kwa mara .

Mnorway Ingrid Kristiansen –binadamu pekee aliewahi kushinda London,NY,Chicago na Boston marathon ameungamkono fikra hii.

Bila ya shaka itakaribishwa pia na majogoo wa mbio hizi hasa kutoka Kenya na Ethiopia.

Mkenya Martin Lil alishinda wiki iliopita London marathon akimpiku bingwa wa rekodi ya dunia wa Berlin,Paul Tergat.

Upande wa wanawake,mshindi alikuwa Radcliffe tena kwa mara ya tatu mfululizo.

TUMALIZIE MBIO ZA MAGARI:

Michael Schumacher na gari lake la Ferrari wanahitaji ushindi kesho huko San Marino .

Mwaka jana Schumacher ,aliwasili Imola,nyumbani mwa Ferrari, akiongoza kuelekea ubingwa wake wa 7 wa Formula one baada ya ushindi 3 mfululizo.Msimu huu haukuanza vyema kwa Schumacher na Ferrari.Kwani, Schumacher yuko pointi 24 nyuma ya Mspain Fernando Alonso anaendesha gari la Renault.Magari ya ferrari yalioshinda mashindano 15 kati ya 18 yaliopita yameshindwa katika mbio 4 mfululizo zilizopita na yanasimama nafasi ya 6 katika orodha ya kuania ubingwa.

Kesho kwahivyo, macho yatakodolewa tena kwa Michael Schumacher kubadili mkondo na mkosi uliompata hadi sasa mwaka huu na gari lake la ferrai.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW