1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Muongozo wa matumizi ya akili mnemba

10 Septemba 2024

Mkutano wa kilele wa kimataifa unaondelea Korea Kusini umetangaza "muongozo wa hatua" zitakazosimamia matumizi na uwajibikaji wa akili mnemba katika jeshi.

Roboti
Teknolojia ya akili mnemba katika matumizi ya kijeshi.Picha: PIERRE ALBOUY/REUTERS

Mpango huo pia unatoa muongozo wa vitendo zaidi kuliko waraka sawa uliotolewa mwishoni mwaka jana, lakini bado hauna nguvu ya kisheria. 

Mkutano wa akili mnemba unaoshughulikia uwajibikaji katika matumizi ndani ya jeshi (REAIM) unaoendelea mjini Seoul, ni wa pili wa aina yake, na unafuatia ule ulifanyika mjini Amsterdam, Uholanzi, mwaka jana.

Wakati wa mkutano huo wa Amsterdam, karibu mataifa 60 yaliidhinisha kwa kiasi fulani "wito wa kuchukua hatua" bila ya kuwekwa mafungamano ya kisheria.

Soma pia: Uingereza yaungana na Ulaya na Marekani kusaini mkataba wa Akili Mnemba

Haijabainika mara moja ni mataifa mangapi kati ya 96 ambayo yalituma wawakilishi wa serikali kwenye mkutano huo, yakiwemo Marekani na China, wameidhinisha waraka huo.

Wakizungumza kwenye meza ya duara leo Jumanne, wawakilishi wa serikali mbalimbali  wamesema "muongozo" wa mwaka huu umejikita zaidi katika kutoa mwelekeo zaidi wa vitendo.

Soma pia: Teknolojia ya Akili Mnemba kusaidia kuhifadhi nyaraka za enzi ya ukoloni

Hatua hii inaendana na maendeleo katika majadiliano kuhusu athari za akili mnemba, na maendeleo katika matumizi ya teknolojia hiyo katika jeshi kama vile hatua ya Ukraine kuzindua droni zinazoweza kutumia akili mnemba.

Uelewa wa pamoja

Serikali zitatathmini za aina ya hatari, na masuala muhimu kama vile udhibiti wa binadamu, na jinsi hatua za kujenga imani zinaweza kuchukuliwa ili kusimamia hatari hizo.Picha: Marc Asensio/NurPhoto/IMAGO

Waziri wa Ulinzi wa Uholanzi Ruben Brekelms akizungumza na shirika la habari la Reuters amesema wamepiga hatua madhubuti zaidi mwaka huu ikizingatiwa kuwa mwaka jana walijadili kuhusu kuunda uelewa wa pamoja.

Hii ni pamoja na kuweka tathmini za aina ya hatari, na masuala muhimu kama vile udhibiti wa binadamu, na jinsi hatua za kujenga imani zinaweza kuchukuliwa ili kusimamia hatari hizo.

Miongoni mwa maelezo yaliyoongezwa kwenye waraka huo ni haja ya kuzuia akili mnemba isitumike na makundi yakiwemo ya kigaidi kueneza silaha za maangamizi makubwa, na umuhimu wa kudumisha udhibiti na ushiriki wa binadamu katika matumizi ya silaha za nyuklia.

Soma pia: Viongozi wa G7 kujadili uhamiaji, Afrika na akili mnemba

Maafisa wa Korea Kusini wamesema waraka huo unashughulikia masuala mengi ya msingi sawa na kanuni zilizowekwa mahali pengine,  kama vile tamko la serikali ya Marekani juu ya matumizi ya uwajibikaji ya akili mnemba katika jeshi lililozinduliwa mwaka jana.

Lakini mkutano wa kilele wa Seoul ulioandaliwa pamoja na Uholanzi, Singapore, Kenya na Uingereza unalenga kuhakikisha unaendeleza mijadala ya wadau wengi isiyotawaliwa na taifa moja au chombo.