Mursi kuchunguzwa kwa madai ya kutoroka jela
12 Julai 2013Mwendesha mashitaka mkuu wa Misri Hesham Barakat amepokea ushahidi kutoka mahakama moja ya mjini Ismailia ambao utatumika kama msingi wa uchunguzi utakaoendeshwa na waendesha mashitaka kwamba Mursi na viongozi wengine zaidi ya 30 wa udugu wa kiislamu walitoroka jela.
Hayo ni kulingana na maafisa wa usalama ambao hawakutaka majina yao yatajwe kwa sababu hawaruhusiwi kuzungumza na waandishi wa habari.Suala la iwapo Hamas liliwasaidia kutoroka wakati wa ghasia zilizokumba wimbi la mageuzi la mwaka 2011 lililomg'oa madarakani Hosni Mubarak limekuwa likijadiliwa kwa miezi kadhaa na limekuwa kidonda ndugu kisiasa kwa Mursi wakati wa utawala wake wa mwaka mmoja kama Rais wa kwanza aliyechaguliwa kwa njia huru na ya haki.
Mashitaka ya uhaini yamkodolea macho Mursi
Wakosoaji wake na idara ya mahakama zimekuwa zikidokeza kuwa ushahidi wa kuwa kulikuwa na muingilio wa kutoka nje nchini Misri huenda ukasababisha mashitaka ya uhaini.
Umuhimu wa suala hilo umeongezeka tangu Mursi kuondolewa madarakani na jeshi mnamo tarehe 3 mwezi huu kufuatia misururu ya maandamano ambayo mamilioni ya wamisri walimtaka ajiuzulu. Tangu hapo kiongozi huyo amekuwa akizuiliwa mahali pasipojulika na bado hakuna mashitaka dhidi yake ambayo yametangazwa.
Kundi la Hamas limekanusha kuhusika katika kisa hicho cha kutoroka jela kilichotokea katika jela ya Wadi el Natroun kaskazini magharibi mwa Cairo.Mursi na viongozi wengine wa udugu wa kiislamu wamesema walisaidiwa na wakaazi wa eneo hilo kutoroka baada ya wengi wa wafungwa kutoroka jela hiyo.
Uchunguzi huo unachipuka kutokana na kesi dhidi ya mfungwa wa zamani lakini jaji Khaled Mahgoub aliigeuza kesi hiyo kuwa uchunguzi wa umma kuhusiana na kutoroka kwa Mursi na maafisa wengine.Maafisa kadhaa wa magereza,polisi na maafisa wa kijasusi wametoa ushahidi mwingine katika vikao vya faragha.
Mwisho wa kesi hiyo jaji huyo aliwasilisha ushahidi aliokusanya kwa mwendesha mashitaka mkuu na kuomba alichunguze suala hilo kwa kina.Kesi hiyo ya Ismailia inatoa taswira kamili ya uhusiano hasi uliokuweko kati ya Mursi na idara ya mahakama iliyomshutumu Rais huyo kwa kuingilia uhuru wa idara hiyo.
Kundi la Hamas lashutumiwa
Maafisa kadhaa wakuu wa polisi na maafisa wa upelelezi wamelilaumu kundi la Hamas ambalo ni mshirika wa karibu wa udugu wa kislamu kwa kuwatuma wapiganaji wake katika ukanda wa Gaza kujiunga na wale wa Bedoiun kutoka rasi ya Sinai na kuvamia magereza na kuwaachilia wanachama wake.
Taarifa hizo za kuanzishwa uchunguzi zinakuja siku moja baada ya maafisa wa usalama kutoa vibali vya kumamatwa kwa kiongozi wa kidini wa Udugu wa kiislamu Mohammed Badie na viongozi wengine tisa kwa tuhuma za kuchochea ghasia baada ya makabiliano ya Jumatatu yaliyosababisha vifo vya watu 51.
Hatua hiyo inaonekana kuwa mipango ya hivi punde kabisa ya jeshi kulikandamiza kundi hilo na kampeini zake za kutaka kumrejesha Mursi madarakani.Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki Moon ameelezea wasiwasi wake kuhusiana na ukandamizaji huo wa udugu wa kiislamu.
Mwandishi: Caro Robi/ap
Mhariri: Gakuba Daniel