Mursi kukutana na Angela Merkel
30 Januari 2013Rais Mohammed Mursi alikuwa amepanga kufanya ziara ya siku mbili hapa Ujerumani na kisha kuelekea Ufaransa siku ya Ijumaa. Lakini sasa safari ya Ufaransa imefutwa na muda wa ziara ya Ujerumani kupunguzwa. Inatarajiwa kwamba Mursi atakuwepo Berlin kwa muda wa masaa machache tu. Mursi amepangiwa kukutana na Kansela Angela Merkel na vile vile atafanya mazungumzo na wawakilishi mbali mbali kutoka sekta ya biashara kwani nchi yake inakumbwa na mgogoro wa kiuchumi. Lengo la Mursi ni kutafuta wawekezaji watakaosaidia kuokoa uchumi wa nchi yake.
Akizungumza katika kituo cha televisheni cha ARD cha hapa Ujerumani, waziri wa mambo ya nje wa nchi hii Guido Westerwelle, amezitaka nchi nyingine ziwe na subira juu ya suala la Misri: "Misri ni mshirika wetu muhimu na ni nchi iliyowezesha mapinduzi katika ulimwengu wa Kiarabu kutokea. Ninashauri tuonyeshe uvumilivu kwa Misri. Tuseme tunachotaka kukosoa lakini tusiache kufanya mazungumzo. Mazungumzo ni njia bora zaidi ya ushawishi."
Westerwelle amesema kuwa Ujerumani itatoa msaada kwa Misri iwapo tu nchi hiyo itafuata masharti fulani. Msaada utategemea kama patakuwa na maendeleo ya kidemokrasia. Westerwelle ameitaka serikali ya Misri kukaa pamoja na wapinzani na kufanya mazungumzo.
Hali ya uchumi bado ni tete
Safari ya Mursi inakuja wakati ambapo maandamano dhidi yake bado yanaendelea Misri. Watu 52 walipoteza maisha yao katika vurugu zilizotokea wakati wa maadhimisho ya miaka miwili baada ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani Hosni Mubarak.
Tatizo kubwa linaloikabili Misri kwa sasa ni la kiuchumi. Idadi ya watalii imepungua kwa kiasi kikubwa baada ya mapinduzi kutokea mwaka 2011. Hivi sasa Misri inahitaji wawekezaji kutoka nje. Hapa Ujerumani, wafanyabiashara wanaelewa kwamba Misri ni mahala pazuri pa kuwekeza lakini wanahofia hali ya usalama.
Mtaalamu kutoka taasisi ya biashara na viwanda Ujerumani, Steffen Behm, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba makampuni ya Ujerumani yanangojea kwanza hali ya kisiasa itulie kabla ya kuwekeza kiasi kikubwa cha fedha nchini Misri.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani anayemaliza muda wake, Bi Hillary Clinton, amesema kuwa kuvunjika kwa uchumi wa Misri kutakuwa na athari kubwa katika maeneo mengi.
Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf