1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni aapa kuendeleza mradi wa mafuta licha ya ukosoaji

Daniel Gakuba
17 Septemba 2022

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ameapa kuendelea na mradi wa bomba la mafuta la Afrika Mashariki, na kupuuza azimio la Bunge la Ulaya lililotaka mradi huo uahirishwe kwa tuhuma kuwa unakiuka haki za binadamu.

Uganda Ölförderung Umwelt Indigene Total
Matayarisho ya awali yako mbioni kwa ujenzi wa bomba la EACOPPicha: Jack Losh

Akizungumza Ijumaa, siku moja baada ya bunge la Umoja wa Ulaya kulipitisha azimio lake, Rais Museveni amesema kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya TotalEnergies ilimshawishi kujenga bomba hilo la mafuta, na kwamba ikiwa itasalimu amri mbele ya shinikizo la Bunge la Ulaya, Uganda itatafuta mshirika mwingine.

Soma Zaidi: Bomba la mafuta la Afrika Mashariki lakabiliwa na mtikisiko

Hayo Museveni ameyabainisha kupitia mtandao wa twitter, na kuongeza kuwa ujenzi wa bomba hilo utaendelea kwa mujibu wa makubaliano na kampuni ya TotalEnergies pamoja na Kampuni ya Taifa ya China ya uchimbaji wa mafuta ya visima vya nchi kavu (CNOOC).

Mapema mwaka huu, kampuni hizo mbili zilisaini mkataba wenye thamani ya dola bilioni 10, ya kujenga bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1, 445 kutoka visima vya mafuta nchini Uganda hadi kwenye bandari ya Tanga nchini Tanzania.

Marais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania (kushoto) na Yoweri Museveni wa Uganda walisaini makubaliano ya kuanza ujenzi wa bomba la EACOP Aprili 2021.Picha: Presidential Press Unit/Uganda

Vipingamizi tangu mwanzoni

Tangu kuanzishwa kwake, mradi huo umekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanaharakati wa mazingira na wa haki za binadamu, wanaosema kwamba unatishia maisha ya makumi kwa maelfu ya watu na mfumo tete wa bioanwai katika ukanda huo.

Azimio lililopitishwa na Bunge la Ulaya siku ya Alhamisi lilielezea wasiwasi juu ya visa vya ''uvunjifu wa haki za binadamu'' katika nchi za Uganda na Tanzania, unaohusishwa na mradi huo wa uwekezaji katika uchimbaji na usafirishaji wa mafuta.

Soma zaidi: Uganda yafunga kazi za mashirika 54 yasiyo ya kiserikali

Visa hivyo ni pamoja na ''kufungwa kinyume cha sheria kwa watetezi wa haki za binadamu, kusimamisha shughuli za asasi za kiraia, na kufurushwa kwa mamia ya watu kutoka katika mashamba yao bila fidia ya kutosha''.

Bunge la Ulaya lilisema watu zaidi ya 100,000 wanakabiliwa na hatari ya kuhamishwa kupisha Bomba la Mafuta la Afrika Mashariki (EACOP).

Shinikizo dhidi ya makampuni ya nishati

Azimio la bunge hilo la Ulaya limeitaka kampuni ya TotalEnergies kusubiri mwaka mmoja kabla ya kuanza ujenzi wa bomba hilo, ili kufanya utafiti wa njia mbadala ''itakayolinda vyema mfumo tete wa bioanwai na vyanzo vya maji nchini Uganda na Tanzania''.

Watetezi wa mazingira wanasema ujenzi wa bomba la EACOP utaathiri sana mfumo wa bioanuai.Picha: Jack Losh

''Kwa njia moja au nyingine, tutaanza kusafirisha mafuta mwaka 2025 kama ilivyopangwa, kwa hiyo, watu wa Uganda wasiogope chochote,'' amesisitiza Rais Museveni katika ujumbe wake.

Mradi huo wa mafuta unanuia kuchimba mafuta ghafi kutoka Ziwa Albert lenye urefu wa kilomita 165 likiwa mpakani kati ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Inakadiriwa kuwa eneo hilo lina hazina ya mapipa bilioni 6.5 ya mafuta ghafi, yapatayo bilioni 1.4 yakiwa katika hali ya kuweza kuchimbwa hivi sasa.

Wabunge wa Uganda wapinga kuingiliwa uhuru wa nchi yao

Azimio la Bunge la Ulaya liliwakasirisha wabunge wa Uganda, na naibu spika wa Bunge la Uganda Thomas Tayebwa alisema hawawezi kuchukulia kwa urahisi hatua hiyo aliyosema inaingilia uhuru wa Uganda.

Wafanyakazi wa ujenzi wa bomba la EACOP, Waganda na Wachina wakijipumzisha baada ya kazi ngumuPicha: Jack Losh

''Huu ni mradi ulioidhinishwa na Bunge la Uganda, bunge la nchi Huru,'' alisema Tayebwa.

Soma zaidi: Samia, Museveni watia dole ujenzi wa bomba la mafuta

Hata hivyo, kundi la watetezi wa mazingira la nchini Ufaransa lilisifu azimio la Bunge la Ulaya, likisema limepeleka ujumbe mzito kwa wanasiasa. Kiongozi wa kampeni wa kundi hilo la Friends of Earth France, Juliette Renaud alisema katika taarifa yake kuwa gharama wa mradi wa EACOP ''kwa binadamu, mazingira na hali ya hewa haiwezi kupuuzwa wala kukubaliwa.''

Kampuni ya TotalEnergies imesisitiza kuwa imechukua hatua za kupunguza athari za mradi huo kwa binadamu na mazingira.

 

~Vyanzo: afpe, ape

     

     

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW