Museveni aendelea kuongoza matokeo ya urais
2 Machi 2016Siku ya Ijumaa (19 Februari), kiongozi wa upinzani na mgombea urais Kizza Besigye alichukuliwa tena na polisi, huku wafuasi wake wakishambuliwa kwa marungu, mabomu ya machozi na risasi za mpira katika mji mkuu, Kampala.
Marekani, ambayo hutoa msaada mkubwa wa kifedha sambamba na mafunzo ya kijeshi kwa Uganda, ililaani vikali mashambulizi hayo dhidi ya wapinzani wa serikali. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, anasema alimpigia simu Rais Museveni kuelezea kutoridhishwa kwa nchi yake na namna ambavyo vyombo vya usalama vimekuwa vikiwatendea wapinzani.
Upigaji kura uliofanyika siku ya Alhamis uliongezewa muda wa siku moja kwa wilaya mbili ambako awali karatasi za kura na baadhi ya vifaa ya uchaguzi hazikuwa zimewasili kwa wakati muafaka.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa saa 7:30 usiku kwa majira ya Afrika Mashariki, Rais Museveni alikuwa anaongoza kwa kura 3,373,998 sawa na 60.8% ya kura zilizohesabiwa, huku mshindani wake wa karibu, Besigye, akiwa na kura 1,932,323 sawa na 34.8%, akifuatiwa na Amama Mbabazi mwenye kura 91,980, yaani 1.7%.
Hii ni kutokana na kura 5,545,099 zilizohesabiwa kwenye vituo 15,801 sawa na 56.41% ya vituo 28,010. Ikilinganishwa na kura zilizotangazwa rasmi saa 4:00 za usiku, Museveni ameshuka kwa asilimia chache, kwani alikuwa na 61.27, huku Besigye akiwa ameongeza angalau asilimia 0.3.
Mbabazi ashindwa kufua dafu
Kinyume na matarajio ya wengi kwamba Mbabazi angechangia katika kumkosesha Rais Museveni ushindi wa moja kwa moja, waziri mkuu huyo wa zamani ameshindwa hata katika wilaya alikozaliwa ya Kanungu, ambako anashikilia nafasi ya tatu. Rais Museveni ndiye aliyeshinda katika wilaya hiyo ya Kanungu akifuatwa na Besigye.
Mwandishi wa DW mjini Kampala Emmanuel Lubega, anaripoti kwamba kwa upande wa wagombea wa viti vya ubunge, mawaziri kadhaa pamoja na wabunge maarufu wamepoteza viti vyao, wakiwemo wa upinzani.
Miongoni mwa mawaziri hao ni Kahinda Otafire wa Masuala ya Katiba; waziri wa nishati na maadini Irene Muloni naye ameshindwa katika jimbo la Bulambuli Mashariki, waziri wa nchi wa makao Sam Engola, waziri wa nchi wa masuala ya kiuchumi Henry Banyenzaki, Sarah Opendi pamoja na Jessica Alupo wa elimu.
Vile vile, uchaguzi huu umewaibua wabunge huru wengi wasio na mafungamano na chama chochote cha kisiasa wakiwa wameshinda mkiwemo wale walioshindwa kwenye kura za mchujo kwenye ngazi za vyama, hasa chama tawala, NRM. Miongoni mwao, ni waziri wa ardhi, Ida Nantaba, aliyeshinda wilayani Kayunga.
Kwa mujibu wa katiba ya Uganda, matokeo yote yanatakiwa yawe tayari ndani ya masaa 48 baada ya kumalizika upigaji kura, kwa hivyo inatazamiwa kuwa hadi jioni ya Jumamosi (Februari 20), tayari matokeo kamili yatakuwa yameshafahamika.
Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa
Mhariri: Caro Robi