1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni amsifia Muhoozi kuwa mwanajeshi shupavu

30 Aprili 2024

Kwa mara ya kwanza, Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemsifu waziwazi mwanawe, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, akimtaja kuwa mzalendo aliye na azma ya kuboresha jeshi la Uganda, akionekana kumpigia debe kumrithi.

Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.
Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba.Picha: Ugandan Presidential Press Unit

Kwenye sherehe ya familia ya maadhimisho ya miaka 50 ya kuzaliwa kwa Muhoozi, Rais Museveni kama baba hakuzuwia hisia zake kumsifu mwanawe kuwa mzalendo na shujaa anayependa sana kuboresha jeshi la Uganda licha ya ukosoaji kutoka ndani na nje ya utawala wake. 

"Watu wamekuwa wakimsema sana Muhoozi… Muhoozi hiki, Muhoozi hili…Aliporudi kutoka mafunzo ya kijeshi, alichangia pakubwa kuboresha jeshi letu kwa sababu yeye anazingatia uzalendo na maslahi ya wanajeshi wala si kazi au utajiri. Ni kuhusiana na hayo ndipo wanajeshi wengi Afrika hupotoka." Alisema kiongozi huyo wa Uganda, akiwa amevalia koti la gwanda la kijeshi.

Soma zaidi: Matamshi ya Jenerali Kahinda yazusha mjadala Uganda

Yumkini hii ndiyo  mara ya kwanza Rais Museveni kutamka waziwazi mtazamo wake chanya kuhusu mwanawe kujiunga na jeshi na pia siasa, baada ya miezi kadhaa tangu amkaripie kwa kusambaza ujumbe usiostahili kwenye ukurasa wake wa X (iliyokuwa Twitter) hasa pale alipoandika kwamba angeliivamia Kenya. 

Imani mpya kwa Muhoozi

Kulingana na wadasisi wa masuala ya kisiasa, sasa Museveni amedhihirisha kuwa anamwamini sana mwanawe katika mazingira ya sasa ya kisiasa na utawala.

Mkuu wa Majeshi wa Uganda, Jenerali Muhoozi Kainerugaba (kushoto) akikata keki ya siku yake ya kuzaliwa akiwa na mkewe, Charlotte, mama yake, Janet, na baba yake.Picha: Ugandan Presidential Press Unit

Kwa hiyo si ajabu kwamba aliamua kumteua kuwa mkuu wa majeshi ili aweze kudhibiti vilivyo usimamizi wa jeshi hilo.

Wambete Wamoto, mchambuzi wa masuala ya ksiasa na kijeshi jijini Kampala, aliiambia DW kwamba Rais Museveni anawahofia sana majenerali wengine ambao hawakubaliani naye na "ndiyo maana anahisi kupata kitulizo mwanawe akiwa mkuu wa majeshi yote."

Soma zaidi: Vuguvugu la MK la Uganda lajigeuza asasi ya kiraia

"Lakini pia afahamu kuwa wengi walijiunga na jeshi lake la waasi wakitokea Chuo Kikuu cha Makerere. Hawakutarajia kujitajirisha lakini kupigania na kulinda haki za binaadamu," alisema Wamoto.

Mchambuzi mwengine, John Kibego, anasema Uganda imeshuhudia jinsi Muhoozi alivyopandishwa vyeo haraka haraka hadi kufikia ngazi ya jenerali na mkuu wa majeshi yote.

"Kwa hivyo, baba yake ameonesha kuwa mwanawe ni mwaminifu na mchapakazi kuliko wengine,” anaongeza.

Ufisadi jeshini

Mara kwa mara, kumekuwepo na habari kwamba maafisa wa ngazi za juu wa jeshi huhusika katika vitendo vya ulaji rushwa na ufisadi kwa jumla.

Rais Yoweri Museveni wa Uganda (kushoto) na mke wake, Janet, wakiinuwa gilasi kusherehekea miaka 50 ya kuzaliwa kwa mtoto wao, Muhoozi Kainerugaba.Picha: Ugandan Presidential Press Unit

Wakati mmoja askari walioko Somalia walilalamikia kupunjwa chakula huku maafisa hao wakiuza bidhaa hizo.

Kwenye sherehe ya siku ya Jumatatu (Aprili 29), Rais Museveni alitamka kuwa mwanawe hajitakii makuu kama wanajeshi wengine.

Soma zaidi: Museven akataa mwanae kujiuzulu

“Watu wengi barani Afrika hujiunga na jeshi wakitaka kazi ya kutajirika haraka. Hiyo ni hatari sana kwa mwanajeshi yeyote.” Alisema.

Jenerali Muhoozi aliteuliwa kuwa mkuu wa majeshi mwezi Machi 2024. Kabla ya hapo alikuwa anashikilia wadhifa wa mshauri mkuu wa rais kuhusiana na masuala ya kiusalama. Hii ilikuwa baada ya kuondolewa kwa wadhifa wa kamanda wa jeshi la nchi kavu. 

Katika kipindi hicho, pia jenerali huyo aliendesha mikutano kadhaa ya hadhara akinadi uzalendo chini ya kundi lake la PLU lililodaiwa kuwa na nia ya kuendesha kampeni za kumpigia debe amrithi baba yake.

Hata hivyo, jambo hilo limepigwa na baadhi ya viongozi wa chama tawala, hasa jenerali Kahinda Otafire, wakisema kuwa "urais wa Uganda si wa kurithishwa."