1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni amteua mwanawe mkuu wa jeshi

24 Juni 2021

Hatua ya rais Yoweri Museveni kumteua mwanawe kuwa kamanda wa majeshi ya ardhini imeibua mjadala mkubwa nchini Uganda. Baadhi wanahisi huu ni muendelezo wa mchakato wa kumuandaa kumkabidhi madaraka pale atakapostaafu.

Uganda Muhoozi Kainerugaba
Picha: Getty Images/AFP/P. Busomoke

Lakini wengine wanahoji kuwa Luteni Jenerali MuhooziKainerugaba amepitia ngazi zote za kijeshi kufikia hapo sambamba na cheo na ujuzi wake.

Habari za rais Yoweri Museveni kumchagua mwanawe luteni jenerali Muhoozi Kainerugaba kuwa kamanda wa jeshi la ardhini hazijaleta mshangao mkubwa kwa baadhi ya watu waliobashiri tangu hapo awali kuwa anamwandaa kumrithi nafasi ya rais.

Ila kinachowakera wengi ni kwamba mtawala huyo wa Uganda tangu mwaka 1986 atakuwa amegeuza nafasi ya kisiasa kuwa ya urithi. 

Wengi husema huyo mwanawe ndiye atakamrithi Museveni

Wakati mmoja akizungumza na DW, Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba alikanusha madai kuwa babake anamwandaa kumrithi.

Rais wa Uganda Yoweri MuseveniPicha: Tanzania State House/Xinhua News Agency/picture alliance

Lakini kila wakati mjadala wa nani atakayemrithi Museveni ukitokea, wengi humnyooshea kidole bwana huyo mwenye umri wa miaka 47.

Wengine hawataki suala hilo la kumteua kwa wadhifa wa kamanda wa majeshi ya ardhini kuwa la kisiasa kwani ana tajriba ya kutosha. Isaac Khisa ni mwanahabari.

Hali hii wakati mwingine imedaiwa kuleta mabishano miongoni mwa viongozi wa chama tawala na uongozi wa ndani wa rais Museveni.

Lakini mwenendo wa kuwateua wakuu wa majeshi kuwa mawaziri kama ilivyokuwa kwa marehemu Jenerali Aronda Nyakayirima, Jenerali Katumba Wamala na hivi karibuni Jenerali David Muhoozi waweza pia kuzingatiwa kuwa mfumo wa Museveni kuwavutia wanajeshi Zaidi katika siasa na moja kwa moja katika shughuli za serikali kwani amekariri kuiamini taasisi hiyo kuliko zingine zote.

Luteni Peter Elwelu ndiye atakayekuwa naibu mkuu wa majeshi

Katika uteuzi uliotangazwa leo, aliyekuwa mlinzi wa rais Museveni wa siku nyingi Wilson Mbadi ndiye ameteuliwa kuwa mkuu wa majeshi.

Kikosi cha jeshi la UgandaPicha: DW/E. Lubega

Luteni Jenerali Peter Elwelu ambaye aliongoza uvamizi wa kasri ya ufalme wa Rwenzururu ambaye amekuwa kamanda wa majeshi ya ardhini ndiye atakuwa naibu wa mkuu wa majeshi.

Hadi kuteuliwa kwake mwanawe Museveni ndiye alikuwa kamanda wa kikosi maalumu cha ulinzi wa rais SFC.