1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni amuondoa mwanae ukuu wa jeshi, ampandisha cheo

4 Oktoba 2022

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amemwondoa mtoto wake Jenerali Muhoozi Kainerugaba kwenye wadhifa wa kamanda wa jeshi la nchi kavu na wakati huo huo kumpandisha cheo kuwa jenerali kamili.

Uganda Kampala | Muhoozi Kainerugaba
Picha: Peter Busomoke/AFP/Getty Images

Jenerali Muhoozi Kainerugaba ameshikilia wadhifa wa kamanda wa jeshi la nchi kavu kwa muda wa miaka miwili na mojawapo ya operesheni maarufu alizoongoza ni ile ya shujaa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kamanda wa operesheni hiyo meja jenerali Kayanja Muhanga ndiye amechukua nafasi hiyo sasa kwa mujibu wa taarifa iliyosambazwa Jumanne alasiri.

Soma pia: Museven akataa mwanae kujiuzulu

Haijafahamika kama rais Yoweri Museveni amechukua hatua ya kumwondoa mwanawe kwenye wadhifa wa kamanda wa jeshi la nchi kavu baada ya yeye kusambaza ujumbe ulioshtumiwa na raia wengi wa Kenya na Uganda kwenye mitandao ya kijamii.

Ujumbe huo umeibua hisia mseto za hasira na kejeli kutoka kwa raia wa nchi hizo mbili, wakati rais William Ruto wa Kenya akitarajiwa kufanya ziara rasmi Uganda wiki hii.

Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni amemuondoa mwanae Muhoozi Kainerugaba kwenye ukuu wa jeshi la ardhini lakini wakati huo huo akampandisha cheo kuwa Jenerali kamili.Picha: ABUBAKER LUBOWA/REUTERS

Katika mfululizo wa ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa tweeter, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto wa rais Museveni amesambaza taarifa ambazo zinagusia ubabe wa kijeshi ilio nao Uganda dhidi ya Kenya na pia kuhusu dhana ya mageuzi ya kisiasa anayoamini inaweza kuzifanya nchi hizi mbili kuwa nchi moja katika muda wa wiki mbili tu.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Uganda imelazimika kuwasilisha taarifa ya kuomba radhi kutoka kwa ile ya Kenya ikisisitiza kuwa ujumbe huo ni maoni ya mtu binafsi wala si msimamo wa taifa la Uganda.

Kinaya cha kumwondoa jenerali huyo kwenye wadhifa wa kamanda wa jeshi la nchi kavu na kisha kumpandisha cheo kimeibua mitazamo kwamba sasa atakuwa na uhuru wa kujishughulisha na siasa bila kuvunja sheria za kijeshi.

Tayari kuna vuguvugu linaloendeleza kampeni za yeye kugombea urais mwaka 2026.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW