1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni ateua wanawake zaidi katika Baraza lake la Mawaziri

9 Juni 2021

Hatua ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kuwateua wanawake wengi kwenye baraza lake la mawaziri ikilinganishwa na serikali zake za awali imepokelewa kwa maoni mseto na mshangao na mashaka.

Uganda Präsident Yoweri Museveni
Picha: Hannah McKay/Getty Images

Miongoni mwa nyadhifa za uwaziri ambazo rais Museveni amewateua wanawake ni ile ya makamu wa rais na pia waziri mkuu. Makamu wa rais ni meja mstaafu Jessica Alupo aliyewahi kushikilia wadhifa wa waziri wa elimu katika serikali ya awamu ya nne ya rais Museveni, lakini pia alikuwa mmoja kati ya walinzi wake kabla ya kustaafu jeshi.

Waziri mkuu ambaye atakuwa kiongozi wa shughuli za serikali ni mfuasi wa dhati wa chama cha NRM. Kwa jumla kati ya mawaziri 80 kwenye baraza hilo idadi ya wanawake ni 35 na wanashikilia wizara muhimu. 

Muundo wa baraza jipya pia unaonesha kuwa Museveni amewaacha nje mawaziri wake wanaoweza kuelezewa kuwa wa kijadi. Hadi 11 kati ya wale ambao siku zote wamekuwa katika serikali yake wametupwa nje hali ambayo inaleta mjadala kama alikuwa hana imani nao tena.

Ikumbukwe kuwa hivi majuzi akilihutubia taifa alitoa tamko kuwa angependa kuwapa nafasi watu ambao si masikini kwa sababu hawawezi kushiriki ufisadi wakitafuta utajiri pamoja na kwamba watoto wa kundi lake alilochukua madaraka nao wamekuja kuwa wazalendo bora.

Bunge la Uganda Picha: DW/Charles Ngereza

Mara nyingi Museveni pia huzingatia kusawazisha uwakilishi wa kanda za nchi katika baraza lake la mawaziri. Kila jamii hufuatilia kuona nani kutoka sehemu yao ameteuliwa.

Watu wa jamii ya Teso ambako makamu mteule wa rais Jessica Alupo anatokea wanaamini kuwa ametimiza ahadi kwao baada ya kanda hiyo kuchagua idadi kubwa ya wabunge wa chama tawala cha NRM badala ya kile cha upinzani cha FDC kama ilivyokuwa katika chaguzi nne zilizopita.

Kwa upande mwingine Museveni amemteua mkuu wa majeshi Jenerali David Muhoozi kuwa waziri kama alivyofanya kwa mtangulizi wake marehemu Aronda Nyakarima. Hii ina maana wananchi watasubiri kuona nani atachukua nafasi hiyo nyeti katika utawala wa muhula wa sita wa Museveni.

Uteuzi wa mawaziri ulikuwa ukisubiriwa kwa hahu na ghamu na wananchi na ulipotangazwa usiku, hali imekuwa na furaha kwa walioteuliwa na wafuasi wao, huku wale waliotupwa nje wakiingiwa na wasiwasi wasijue nini kitakachofuata na bendera za vigogo zikiondolewa kwenye magari yao kuanza maisha ya raia wa kawaida.

Mwandishi: Lubega Emmanuel DW Kampala.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW