Museveni awataka watu wasipeane mkono kuzuwiya Ebola
8 Desemba 2007Matangazo
KAMPALA
Rais Yoweri Museveni wa Uganda amewataka wananchi wake wasipeane mikono ili kujaribu kuzuwiya kuenea kwa homa ya Ebola ambayo imewambukiza watu 101 na kusababisha vifo vya watu 22 nchini humo.
Museveni amekaririwa na gazeti la serikali la New Vision akisema kwamba Ebola huenea kwa kupitia kugusana na kwa wakati huu watu wawe wanasalimiana kwa kupunga mkono tu. Amesema kutompa mtu mkono hakumaanishi kwamba yeye hampendi mtu huyo.
Hapo jana serikali imesema kesi zinazotuhumiwa kuwa za Ebola karibu zote zikiwa katika wilaya ya magharibi ya Bundibugyo yenye kupakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo zimeongezeka na kufikia 101 ikiwa ni pamoja na kesi mbili zilizotokea Kampala ambapo daktari mmoja amekufa.