Museveni: Miaka 30 na bado anataka tena
20 Januari 2016Yoweri Kaguta Museveni alizaliwa Septemba 15, mwaka 1944 katika wilaya ya Mbarara, Uganda na anatokea kabila la Banyankole. Wazazi wa Museveni ni wafugaji na jina lake la katikati alilipata kutoka kwa baba yake, Amos Kaguta, aliyekuwa mchungaji. Museveni amesoma shule ya msingi ya Kyamate na kujiunga na shule ya sekondari ya Mbarara na Ntare.
Mwaka 1967 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambako alichukua masomo ya uchumi na siasa ya sayansi na alifata nadharia za kisoshalisti za Marx, hivyo kujihusisha katika siasa zenye msimamo mkali.
Akiwa chuoni alianzisha kundi la harakati la wanafunzi la African Revolutionary Front na aliongoza ujumbe wa wanafunzi kutembelea maeneo yaliokombolewa na wapiganaji wa chama cha Ukombozi wa Msumbiji cha FRELIMO wakati wa vita dhidi ya ukoloni wa Wareno, ambako alipata mafunzo ya msituni.
Mwaka 1970 Museveni alijiunga na idara ya ujasusi ya Rais Apolo Milton Obote. Wakati Jenerali Idi Amin alivyochukua madaraka Januari mwaka 1971 baada ya kufanya mapinduzi ya kijeshi, Museveni alikimbilia uhamishoni nchini Tanzania ambako alianzisha kundi la Front for National Salvation, lililosaidia kumuangusha madarakani Amin mwaka 1979.
Museveni alishika nafasi mbalimbali katika serikali za mpito na mwaka 1980 aligombea urais wa Uganda, katika uchaguzi ulioonekana kugubikwa na hila na kumpa ushindi Milton Obote. Rais Museveni alianzisha chama cha National Resistance Movement (NRM).
Ajitangaza kuwa rais wa Uganda
Januari 26 mwaka 1986, Museveni alijitangaza kuwa rais wa Uganda. Alichaguliwa kushika nafasi hiyo Mei 9, mwaka 1996 na wafuasi wake wanaomuunga mkono walishinda viti vingi vya bunge katika uchaguzi wa wabunge uliofanyika mwezi uliofuata na hivyo kuliongoza bunge hilo.
Museveni alichaguliwa tena mwaka 2001 na 2006 baada ya katiba kufanyiwa marekebisho na kuondoa muda wa kikomo cha urais. Mwaka 2011 alichaguliwa tena, ingawa upinzani na waangalizi wa kimataifa walielezea kuwepo matatizo katika mchakato wa uchaguzi.
Ingawa, awali Museveni alikataa mfumo wa demokrasia wa vyama vingi, akisema utaitumbukiza nchi hiyo ndogo kwenye siasa za kikabila, alikubali matokeo ya kura ya maoni ya mwaka 2005, ambayo kwa kiasi kikubwa yaliunga mkono kuwepo tena siasa za vyama vingi. Mwaka uliofata Uganda ilifanya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi tangu mwaka 1980.
Museveni na kampeni dhidi ya Ukimwi, LRA
Museveni pia alitekeleza hatua madhubuti za kupambana na UKIMWI, hivyo kuifanya Uganda kuwa nchi ya kwanza barani Afrika kufanikiwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Katika sera zake za kigeni, Museveni mara nyingi amezua utata kwa kuwaunga mkono waasi kwenye nchi nyingine za Afrika. Alimuunga mkono Laurent Kabila, aliyemuondoa madarakani Mobutu Sese Seko mwaka 1997 katika nchi jirani ya Zaire ambayo kwa sasa ni Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Pia alikiunga mkono chama cha RPF, cha waasi wengi wao Watutsi waliokuwa uhamishoni waliopigana dhidi ya serikali ya Rwanda iliyokuwa ikiongozwa na Wahutu.
Aidha rushwa limekuwa suala kubwa katika utawala Museveni. Kwa miaka kadhaa msaada wa kigeni na ndani kwa Museveni ulipungua kiasi, huku rushwa ikichukuliwa kama moja ya tatizo.
Pia Museveni alijikuta kaika wakati mgumu kutokana na kushindwa kulisambaratisha kundi la waasi la Lord's Resistance Army (LRA) linaloongozwa na Joseph Kony, ambalo limekuwa likiendesha mashambulizi kaskazini mwa Uganda.
Mwezi Agosti, mwaka 1973, Rais Yoweri Kaguta Museveni alimuoa Janeth Kataha na wamejaliwa watoto wanne.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman