1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Museveni na Bobi Wine walaumiana kuhusu vifo vya raia

30 Novemba 2020

Rais Yoweri Museveni na mpinzani wake Robert Kyagulanyi wameshtumiana kuhusu nani alaumiwe kuhusu vifo vya watu 54, walipoteza maisha katika ghasia za siku mbili zilizozuka sehemu mbalimbali za nchi.

Bildkombo Yoweri Museveni und Bobi Wine

Rais Yoweri Museveni na mgombea Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine walitoa hotuba zao kwa wakati mmoja. Huku Museveni akiwasiliana kupitia idhaa za televisheni na redio, Bobi Wine alihutubia kupitia kwenye jukwaa la facebook. Katika hotuba zao, wamezidi kushtumiana kuhusu vyanzo na matokeo ya ghasia zilizowasababishia watu 54 kupoteza maisha yao.

Soma zaidi: Uganda: Viongozi wa upinzani wahangaishwa na polisi

Mwanzoni umma ulifahamishwa kuwa hotuba ya rais Museveni ingehusiana na masuala ya kitaifa wala si kisiasa. Lakini mara tu baada ya kuelezea kuhusu hali ya ugonjwa wa COVID-19, rais Museveni alimgeukia mshindani wake mkuu
katika uchaguzi wa mwaka 2021 akimshtumu kwa kuchochea ghasia zilizosababisha vifo hivyo.
Hata hivyo Bobi Wine amekanusha vikali madai ya rais Museveni na shtuma dhidi yake kuwa mtu anayenufaika kisiasa kutokana na ghasia bila kujali maisha na amani ya wafuasi wake na wananchi kwa jumla. Soma zaidi: Maoni: Waganda wamemchoka Museveni lakini hawawezi kumuondoa

Huku akionya kuwa utawala wake umejiandaa vilivyo kukabiliana na watu wanaozingatia kuitumbukiza Uganda katika machafuko kwa visingizio vya kuleta demokrasia, Museveni ameendelea kuwataja watu na mataifa ya kigeni yasiyoitakia Uganda mema kuwa wanashirikiana na upinzani kuvuruga amani na uthabiti katika nchi hii.

Wakati huo huo, serikali ya Uganda imekanusha madai ya ujumbe wa umoja wa Ulaya kwamba safari hii hawakualikwa kushiriki kama waangalizi katika uchaguzi ujao. Katika taarifa iliyotolewa na ujumbe huo, aidha hawaoni manufaa ya kushiriki kwani mapendekezo yao hayajawahi kutiliwa maanani na kutekelezwa katika chaguzi tatu zilizopita.

Watu 54 waliuawa katika maandamano ya wapinzaniPicha: AP Photo/picture alliance

Lubega Emmanuel
DW Kampala.