1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUganda

IGAD wazitaka pande zinazohasimiana Sudan kukutana mara moja

19 Januari 2024

Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Pembe ya Afrika, IGAD imehimiza pande hasimu nchini Sudan kukutana katika muda wa siku 14 zijazo ili kuangazia namna ya kumaliza mzozo baina yao.

Sudan 2019 | Wapiganaji wa kikosi cha Rapid Support Forces
Wanamgambo wa RSF wanaopigana na kikosi cha jeshi cha Sudan wakiwa katika harakati zao katikati ya mzozo baina yaoPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Mwito huo umetolewa kwenye mkutano wa kilele wa IGAD uliofanyika jana mjini Kampala, Uganda.

Mkutano huo wa siku moja uliitishwa chini ya mchakato wa upatanishi wa Jumuiya ya IGAD na unalenga kukomesha vita na janga la kibinadamu.

Viongozi wakuu wa nchi wa wanachama wa IGAD waliohudhuria ni pamoja na mwenyeji Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Salva Kiir wa Sudan Kusini, Hassan Sheikh Mahmoud wa Somalia, Ismail Omar Guelleh wa Djibouti na William Ruto wa Kenya.

Wakuu hao walitoa mwito kwa majenerali hasimu wa Sudan, Abdel Fattah Al-Burhan anayeongoza jeshi la taifa na Mohamed Dagalo anayeongoza kikosi cha wanamgambo wa RSF kukutana ili kumaliza vita na mzozo mkubwa wa kibinaadamu unaoikumba nchi hiyo tangu mapigano yalipozuka Aprili, 2023.

Sehemu ya taarifa ya pamoja iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Djibouti Muhamad Yusuf  alisema "Tunahimiza pande zinazozozana kukutana ana kwa ana katika kipindi cha siku 14. Tunasisitiza kama mataifa ya IGAD kwamba tutatumia mbinu zote ndani ya uwezo wetu kuhakikisha mzozo wa Sudan unatatuliwa kwa njia ya amani."

Soma pia: Sudan yakataa kushiriki mkutano wa IGAD na Kenya

Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat ameahidi kuunga mkono juhudi za kuleta suluhu nchini SudanPicha: Simon Maina/AFP

Wajumbe wengine wa ngazi za juu kutoka Umoja Mataifa, Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya na Muungano wa mataifa ya Kiarabu ikiwemo Misri, Saudi Arabia, Uturuki na Umoja wa Falme za Kiarabu  walihudhuria mkutano na kuwataka majenerali hao kutambua jukumu lao katikati ya hali mbaya ya kibinadamu inayokumba raia wa Sudan.

"Umoja wa Afrika utaheshimu hatua zenu za pamoja za kuwasaidia ndugu zetu wa Sudan kuondokana na mgogoro huu lakini wajibu msingi ni kwa wao wenyewe kuamua hatma ya taifa lao," alisema Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika Moussa Faki Mahamat.

Miito hiyo imetolewa wakati ripoti zikisema mapigano bado yamechacha nchini Sudan kati ya pande hizo mbili. Haijafahamika mara moja iwapo juhudi za IGAD za kuwakutanisha majenerali hao hasimu zitazaa matunda hasa katika wakati ambapo serikali mjini Khartoum ikivutana na jumuiya hiyo.

Mapema wiki hii wizara ya mambo ya kigeni ya Sudan ilisema inasitisha uhusiano na IGAD kufuatia ripoti kwamba ilimwalika kiongozi wa RSF kwenye mkutano wa IGAD mjini Kampala, ingawa hakuonekana wala kuuhutubia mkutano huo.

Jumuiya ya IGAD imeitaka Ethiopia kuheshimu mipaka ya Somalia ili kuepusha mzozo ulioanza kufukuta baada ya makubaliano ya Somaliland na EthiopiaPicha: Reuters/T. Negeri

Kusanyiko hilo pia lilijadili mzozo unaofukuta kati ya Somalia na Ethiopia kuhusu mkataba uliosainiwa hivi karibuni kati ya jimbo lenye utawala wake wa ndani la Somaliland na serikali mjini Addis Ababa la kuipa Ethiopia eneo la bandari.

Wajumbe wameitaka Ethiopia kuufuta mkataba huo na kuiheshimu Somalia na mipaka yake. Mjumbe maalum wa Marekani Mike Hunter ameonya kuwa suala hilo lisipotatuliwa litasababisha mvutano katika eneo la Bahari ya Shamu ambayo ni njia kuu ya kibiashara duniani.

Viongozi na wajumbe hao wameihakikishia Sudan na Ethiopia kuwa wako tayari kusaidia katika kutatua migogoro husika kwani wasipofanya hivyo, kuna hatari ya kanda ya pembe ya Afrika kutumbukia katika vita vya muda mrefu. Hata hivyo, Ethiopia na Sudan hawakuhudhuria wala kutuma wawakilishi.