Museveni na Wine walaumiana kwa kupanga njama za ghasia
2 Januari 2026
Rais Yoweri Museveni anayewania kubakia madarakani na mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi, kila mmoja amemkosoa mwenzake kwa kupanga njama za kusabisha vurugu katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 15 Januari.
Zikiwa zimesalia siku 13 uchaguzi ufanyike Uganda, Rais Yoweri Museveni amedai kuwa mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine amepanga ghasia akisaidiwa na wafadhili wake wa kigeni wasioitakia Uganda mema.
Museveni, Kyagulanyi watupiana lawama
Katika hotuba yake ya mwaka mpya kwa taifa, rais Museveni amemtaja mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi kama mtu ambaye hajakomaa kisiasa na ndiyo maana hazingatii matokeo ya matamshi yake. Kiongozi huyo ambaye ametawala Uganda kwa miaka 40 sasa anakosoa mataifa ya kigeni ambayo yanafadhili kampeni za Bobi Wine akielezea kuwa hayana nia njema kwa Uganda.
Kwa upande wake Bobi Wine amemjibu Museveni akisema kuwa ni wazi kwamba utawala wa Museveni ndiyo umejiandaa kuvuruga uchaguzi kutokana na kanuni ambazo zinazidi kutolewa kama vile kuwakataza watu kubaki kwenye vituo vya kupigia kura kufuatilia zoezi hilo kwa karibu. Msimamo huo wa utawala anaulezea kuwa hila ya kuweza kughushi matokeo na hii inawatishia wapigaji kuhusiana na kushiriki katika uchaguzi.
Katika kipindi cha kampeni, majeshi na polisi wameshuhudiwa wakiwacharaza wafuasi wa upinzani hasa wa chama kikuu cha upinzani cha NUP wakiwa kwenye misafara na mikutano ya kampeni. Museveni amewahimiza kutotumia mbinu hiyo akiwashauri kutumia mabomu ya kutoa machozi lakini pia kwa tahadhari.
Kamatakamata ya wanaharakati yahofiwa kuanza
Kwingineko kamatakamata ya wanaharakati wa haki za binadamu hasa viongozi wa asasi za kiraia inahofiwa kuwa imeanza kutekelezwa.
Kwenye uchaguzi uliopita wanaharakati kadhaa walikamatwa na kuzuiliwa katika kipindi cha uchaguzi. Kukamatwa kwa mwanaharakati maarufu wa masuala ya utawala na demokrasia Sarah Birete siku mbili zilizopita kumetajwa na wenzake kuwa mojawapo na njia za kutaka kuwatishia wasiendelee na shughuli zao za kufuatilia mchakato wa uchaguzi.
Mwito wa wapiga kura kubaki kwenye vituo vya uchaguzi umeungwa mkono pia na viongozi mbalimbali wakiwepo wa kidini. Ikumbukwe kuwa rais Museveni alitoa angalizo kuwa kila mwanajeshi na polisi atakuwa na risasi 120 kwa hiyo watu wasidhani kwamba watawazidi nguvu ikiwa watang'ang'ania kubaki kwenye vituo vya kupigia kura badala ya kurudi nyumbani baada ya kupiga kura.