Musharraf kuendelea kuzuiliwa nyumbani
14 Mei 2013Mahakama hiyo ya mji wa Rawalpindi, karibu na mji mkuu Islamabad pia imesongeza mbele kesi ya kuskiza ombi la kuwachiwa kwa dhamana lililowasilishwa na Musharaf, hadi Mei 20. Mwendesha mashtka Chaudhry Azahr amesema kesi hiyo iliahirishwa baada ya wakili wa Musharraf, Salman Safdar kukosa kufika mahakamani.
Hicho kilikuwa kikao cha kwanza cha kusikizwa kesi hiyo baada ya mwendesha mashtaka mkuu wa serikali anayeshughulikia mauaji ya Bhutto ya mwaka wa 2007 na mashambulizi ya Mumbai mwaka wa 2008, Chaudhry Zulfiqar Ali, kupigwa risasi na kuuawa mjini Islamabad wakati akiwa njiani kuelekea mahakamani mnamo Mei 3.
Musharraf anatuhumiwa kwa kula njama ya mauaji ya aliyekuwa waziri mkuu kwa mihula miwili Benazir Bhutto, ambaye chama chake cha Pakistan Peoples Party - PPP kilipigiwa kura kuingia madarakani Februari 2008 na watu wengi waliosikitishwa na kifo chake. Serikali ya Musharraf ilimshutumu mkuu wa kundi la Taliban nchini Pakistan Baitullah Mehsud, kuhusika na mauwaji hayo, madai ambayo aliyakanusha kabla ya kuuawa katika shambulizi la ndege ya Marekani isiyoruka na rubani mnamo mwaka wa 2008.
Nawaz Sharif apata ushindi mkubwa
Matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu wa Pakistan yamethibitisha ushindi mkubwa kwa chama cha Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharif. Takwimu zilizotolewa hii leo na Tume ya Uchaguzi ya Pakistan zinaonesha kuwa chama cha Pakistan Muslim League-N cha Waziri Mkuu wa zamani Nawaz Sharif kina uwezo mkubwa wa kupata wingi wa viti bungeni, na kumpa fursa ya kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya tatu.
Tume ya uchaguzi imesema chama cha Sharif kimeshinda 123 kati ya viti 272 vya uchaguzi katika bunge la nchi hiyo. Wagombea wasio na vyama ambao kwa kawaida hujiunga na chama ambacho huunda serikali, walishinda viti 25. Hivyo basi jumla ya hesabu ya viti itakipa chama cha Sharif zaidi ya viti 137 vya moja kwa moja kinachohitaji ili kuwa na wabunge walio wengi.
Tume hiyo imesema kuwa chama tawala kinachoondoka madarakani cha Pakistan Peoples Party kimeshidna viti 31 pekee. Chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf kinachoongozwa na nyota wa zamani wa mchezo wa Kriketi Imran Khan kilishinda viti 26.
Khan amesema anapanga kuwasilisha ombi la kuhesabiwa upya baadhi ya matokeo hayo, wakati kundi moja la waangalizi nchini humo likisema baadhi ya vituo vya kupigia kura vilishuhudia idadi kubwa ya wapiga kura kuliko idadi kamili ya watu waliosajiliwa rasmi.
Mwandishi: Bruce Amani/DPA/AFP
Mhariri: Yusuf Saumu