Musiala alenga kurejea uwanjani tena mwaka 2025
3 Septemba 2025
Hii ni baada ya Musiala kuvunjika mguu na kifundo cha mguu katika Kombe la Dunia la Vilabu huko Marekani mnamo mwezi Julai.
Musiala mwenye umri wa miaka 22, alipata jeraha hilo wakati alipogongana na mlinda lango wa Paris Saint Germain wakati huo Gianluigi Donnarumma.
"Mguu unaendelea vyema na unapona kulinganana mpango uliowekwa," Musiala aliliambia jarida la SportBild. "Sihitaji magongo ya kutembelea tena ila sitaki kuharakisha mambo. Nitachukua muda unaohitajika."
"Sitaki kuweka tarehe fulani ila kulingana na hatua nilizopiga, nataka kuichezea Bayern tena mwaka huu wa 2025," alisema Musiala.
Hakuna haja ya kumlaumu Donnarumma
Musiala aliyemaliza msimu uliopita akiwa na mabao 21 na kusaidia kuunda mengine 8, Bayern waliposhinda taji la Bundesiga, hajamlaumu Donnarumma kwa jeraha lake akisema majeraha kama hayo hutokea katika kandanda.
"Kisaikolojia, wiki chache za kwnaza hazikuwa rahisi kwangu. Ila hakuna haja ya kuhuzunika kila wakati," alisema Mjerumani huyo.