Musiala arudi kikosini baada homa
13 Januari 2025Musiala alikosekana katika mechi ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Borussia Mönchengladbach Jumamosi, lakini sasa anatarajiwa kujumuishwa kikosini kwa mechi ya Bundesliga dhidi ya Hoffenheim siku ya Jumatano.
Soma pia:Vilabu vyarejea mazoezini kabla ya kuanza mzunguko wa pili
Bayern wanaongoza Bundesliga kwa pointi nne mbele ya mabingwa Bayer Leverkusen. Penalti ya kipindi cha pili kutoka kwa Harry Kane iliipa Bayern Munich ushindi wa 1-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach siku ya Jumamosi, na kurejesha uongozi wao wa pointi nne kileleni mwa jedwali la Bundesliga.
Gladbach haikuweza kufurukuta mbele katika safu ya ushambuliaji lakini waliwakatisha tamaa Bayern, ambao walidhibiti mchezo lakini kushindwa kupata fursa za kutikisa wavu.
Zikiwa zimesalia zaidi ya dakika 20, Michael Olise aliangushwa kwenye eneo la kisanduku na Lukas Ullrich wa Gladbach, na hivyo kumtoa fursa yengine kwa Kane kuongeza kapu lake la mabao kupitia mkwaju wa penalty.
Kane sasa amefunga penalti 26 mfululizo kwa klabu na nchi na mara ya mwisho alikosa kufunga penalty dhidi ya Ufaransa katika robo fainali ya Kombe la Dunia la 2022.
Je Kocha wa Bayern Vincent Kompany anatarajia nini kwa sehemu ya pili ya msimu?
"Nadhani jambo kubwa zaidi ni kujizingatia sisi wenyewe, kwa kujiandaa kwa mechi moja baada ya nyengine."
"Kuwa na mawazo ya kushinda, na kuwa vizuri katika kila awamu, katika kila jambo tunalofanya. Kutakuwa na wakati mzuri na wakati mbaya lakini nadhani kwa ujumla tulionyesha dalili nzuri."
Matumaini ya Leverkusen kutetea taji la Bundesliga
Mabingwa watetezi Bayer Leverkusen wametulia katika nafasi ya pili kwa jumla ya pointi 35, ikifuatiwa na Eintracht Frankfurt pointi 30 baada ya kuilaza St Pauli bao 1- bila jibu. Kwa mara nyengine tena mshambuliaji Omar Marmoush akiiweka kifua mbele Frankfurt huku kukiwa na tetesi kuwa nyota huyo wa Misri yuko mbioni kuhamia Manchester City.
Bao la 14 kwa Marmoush katika mechi 16 za Bundesliga msimu huu, moja tu nyuma ya Harry Kane.
Katika mechi nyengine, RB Leipzig ilicharaza Werder Bremen 4-2, Stuttgart ikivuna ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya Ausburg.