1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Musiigeuze Mediterenia kuwa bahari ya mauti" - Papa Francis

23 Septemba 2023

Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis, amelaani kile alichokiita "uzalendo wa uadui" na ametaka Ulaya iungane kushughulikia uhamiaji ni kuzuwia kuigeuza Bahari ya Mediterenia kuwa "kaburi la heshima".

Frankreich | Marseille | Papst Franziskus und Emmanuel Macron Treffen
Picha: Andreas Solaro/AFP/AP/picture alliance

Mkuu huyo wa Kanisa Katoliki aliyazungumza kwenye hotuba yake refu ya kuunga mkono kuwakaribisha wahamiaji barani Ulaya iliyohitimisha kongamano la Kanisa lake juu ya masuala ya Bahari ya Mediterenia mjini Marseille, mji wa bandari wa Ufaransa ambao kwa karne kadhaa umekuwa makutano ya tamaduni na dini mbalimbali.

"Kuna kilio cha maumivu kinachotugusa sote, na kinaibadilisha Mediterenia, bahari yetu, kutoka kuwa chanzo cha ustaarabu na kuwa, bahari ya mauti, kaburi la heshima: ni kilio cha masikitiko cha kaka na dada zetu wahamiaji", alisema.

Papa Francis alipokelewa kwenye mji huo na Rais Emmanuel Macron ambaye baadaye walipangiwa kuwa na mkutano wa faragha siku ya Jumamosi (Septemba 23) kabla ya kurejea mjini Roma.

Soma zaidi: Papa Francis ziarani Marseille kujadili mzozo wa wahamiaji

Papa aliianza siku hiyo kwa kukitembelea kituo kinachowahudumia wenye mahitaji katika wilaya ya Mtakatifu Mauront, mojawapo ya maeneo masikini kabisa nchini Ufaransa, kinachosimamiwa na watawa na kilichoanzishwa na Mtakatifu Mama Teresa. 

Papa Francis akizungumza kwenye kongamano la Kanisa Katoliki juu ya masuala ya Bahari ya Mediterenia lililofanyika Marseille, Ufaransa, tarehe 23 Septemba 2023.Picha: Alessandra Tarantino/AP Photo/picture alliance

Baadaye kwenye kongamano hilo, alitowa wito wa kuwepo kwa njia nyingi, za kawaida na za halali kwa wahamiaji, akisisitiza kuwakubali zaidi wale wanaokimbia vita, njaa na umasikini kuliko "kulinda hali ya ustawi wa mtu binafsi."

Wahamiaji 178,500 waingia Ulaya mwaka huu

Kwa mujibu wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR), wahamiaji wapatao 178,500 wameingia barani Ulaya kupitia Bahari ya Mediterenia mwaka huu, huku wengine wapatao 2,500 wakifa ama kupotea.

Serikali za mataifa kadhaa ya Ulaya, zikiwemo za Italia, Hungary na Poland, zinaongozwa na wapingaji wakubwa wa wahamiaji. 

Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa (kushoto) akikamribisha mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, kwenye mji wa bandari wa Marseille.Picha: Andreas Solaro/AFP/AP/picture alliance

Papa Francis alitowa wito kwa watu "kuvisikia vilio vya maumivu" vinavyopazwa kutoka Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Soma zaidi: Papa Francis ayakosoa mataifa ya magharibi

"Ni katika muda kama huu ambapo tunahitaji makutano haya, pale uzalendo wa uadui na usio maana unapotaka kuifanya ndoto ya jamii ya mataifa kufifia," alisema bila kuitaja nchi yoyote kwa jina.

Kiwango cha uwazi alichonacho Papa Francis, ambaye amekuwa akitowa wito kwa mataifa ya Ulaya kugawana wahamiaji, kauli zake dhidi ya kuwatenga wahamiaji kwamba ni "jambo la kashfa, linaloudhi na dhambi" zimewakera sana wanasiasa wahafidhina baranik humo.

Siku ya Ijumaa (Septemba 22), alisema wahamiaji wanaoyaweka hatarini maisha yao baharini "lazima waokolewe" kwani kufanya hivyo "ni wajibu wa kibinaadamu" na kwamba wale wanaozuwia juhudi za uokozi wanaonesha "chuki za wazi."

Chanzo: Reuters
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW