1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musitishwe na magaidi! asema Westerwelle akiwa Morocco

17 Mei 2011

Ujerumani imeutolea wito uongozi wa Morocco kuendelea katika mkondo wa demokrasia hata baada ya shambulio la bomu la kigaidi kutokea nchini humo. Shambulio hilo lilitokea mnamo tarehe 28 mwezi wa Aprili na kuwaua watu 17

Waziri Guido Westerwelle akitembea mjini na Meya Fatima Ezzahra Mansouri mjini MarakkechPicha: picture-alliance/dpa

 Wakati huohuo, Umoja wa Ulaya unalirai eneo la Kaskazini mwa Afrika kuwa na ushirikiano katika suala la nishati kwa minajili ya kuziunga mkono harakati za kudumisha demokrasia kwenye kanda hiyo. Kauli hizo zimetolewa wakati Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle anafanya ziara ya siku mbili nchini Morocco.

Demokrasia iko ngangari

Akizungumza mjini Marrakech, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, alisema kuwa Mfalme Mohammed wa VI alishayatangaza mageuzi ambayo ni sanjari na mabadiliko ya kisiasa.

Mfalme Mohamed VI wa Morocco: Kiongozi tayari ametangaza mageuzi ya kisiasaPicha: Mustpha Houbiss

Kiongozi huyo alimtolea wito Mfalme Mohammed wa VI kutotishwa na magaidi na kwamba Ujerumani na kwamba, "Naipongeza sana serikali ya Morocco ambayo imeweka yote bayana kwa kuanzisha mchakato wa kufanya mageuzi ya kisiasa. Kamwe haipaswi kutishwa na magaidi. Ninaipongeza kwa kweli." alisisitiza.

Shada la maua

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle, aliweka shada la maua kwenye eneo kulikotokea shambulio hilo la bomu la Aprili ili kuwakumbuka waliouawa. Shabaha ya magaidi hao ilikuwa kuushambulia mkahawa mmoja, maarufu kwa watalii, ulioko katikati ya mji mkuu wa Morocco.

Waziri Guido Westerwelle akiweka shada la mauaPicha: picture-alliance/dpa

 Hata hivyo hakuna Wajerumani wowote waliouawa au kujeruhiwa katika shambulio hilo. Kwa sasa, watuhumiwa watatu wa ugaidi walio na msimamo mkali wanazuiliwa tangu mkasa huo utokee.

Ratiba nzito

Dhamira ya ziara ya Waziri Guido Westerwelle ni kuijua sababu na kiini cha maandamano yanayoligubika eneo la Maghreb na ulimwengu wa Kiarabu kwa jumla.

Kwa mujibu wa ratiba iliyoandaliwa, Waziri Westerwelle alikutana na Mfalme Mohammed wa VI kwenye kasri lake la Marrakech na ataelekea hadi mji mkuu wa Rabat atakakofanya kikao na Waziri Mkuu Abbas el- Fassi na mwenzake Taieb Fassi-Fihri.

 Ifahamike kuwa Mfalme Mohammed wa VI ameahidi kuwa atafanya mabadiliko ya katiba yaliyo na azma ya kuyapunguza madaraka yake kwa upande mmoja na kwa upande wa pili, kuuimarisha serikali na bunge kwa jumla.

Kauli hizo zinaungwa mkono na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle: "Matunda ya mageuzi sharti yashuhudiwe kwa mapana na marefu. Kwa hiyo, hilo ndilo suala ambalo lazima tulitie maanani kila wakati kwamba kwa upande mmoja mageuzi ya kidemokrasia yameshika usukani na kwa upande wa pili, mafanikio nayo pia  yatakuwako kwa sababu mchakato huu ni safari ndefu isorudi nyuma."


Wafungwa mapaani

Hata hivyo bado maandamano yanaendelea kuizonga miji kadhaa ya taifa hilo. Hapo jana Jumatatu, kiasi ya watu 324 walishiriki kwenye maandamano yaliyotokea katika jela ya Zaki iliyo karibu na mji mkuu wa Rabat.

Mkahawa uliolipuliwa mjini Rabat tarehe 28 Aprili: 17 waliuawaPicha: AP

Kwa mujibu wa waandamanaji hao, wafungwa wanaozuiliwa kwenye jela hiyo wanateswa na kufanyiwa ukatili. Kutokana na hilo, maafisa wa usalama wa serikali ya Morocco walilazimika kutumia gesi ya kutoa machozi na virungu kuwatawanya waandamanaji hao waliokuwa wameyavamia mapaa ya jela ya Zaki ili kukitoa kilio chao.

Kwa upande wake, serikali ya Morocco inasisitiza kuwa inafuata sheria zilizopo za wafungwa. Ifahamike Morocco inapokea msaada mkubwa kutoka kwa Ujerumani.

Mwandishi: Mwadzaya, Thelma-RTRE/DPAE

Mhariri:Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW