1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Musiwe na hofu! yasema EU kuhusu homa ya Nguruwe

1 Mei 2009

Jamii ya kimataifa inaendelea na harakati za kuwatuliza watu kote ulimwenguni baada ya kuzuka kwa homa ya nguruwe.Homa hiyo iliyozuka mara ya kwanza huko Mexico sasa imesambaa katika mataifa 26 kote ulimwenguni.

Rais wa Mexico Felipe CalderonPicha: AP

Watu 12 tayari wamefariki Mexico kwenyewe na wengine 300 wameambukizwa virusi hivyo.Wakati huohuo Umoja wa Ulaya umeafikiana kushirikiana katika suala la chanjo na dawa za kupambana na homa hiyo kadhalika imepinga hatua ya kupiga marufuku safari za ndege zinazoelekea Mexico.Wafanyabiashara wa nguruwe na bidhaa zake nao wanashikilia sharti jina la homa hiyo libadilishwe ili kuepuka hasara.


Mexico hii leo imeanza rasmi kutimiza marufuku ya siku tano ya kutotoka nje iliyoamrishwa na rais wan chi hiyo Felipe Calderon.Mpaka sasa watu 12 pekee ndio waliofariki na wengine 300 walioambukizwa nchini humo wanaripotiwa kuwa hali nzuri baada ya kupata matibabu.Hatua hiyo ilichukuliwa kwa lengo la kutathmini jinsi virusi vya H1N1 vinavyoendelea kusambaa.Maandamano ya kuadhimisha siku ya wafanyikazi ya leo yamepigwa marufuku huko Mexico.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Ulimwenguni WHO,Margaret ChanPicha: AP

Kwa upande wake Shirika la Afya Ulimwenguni WHO limesisitiza kuwa kuna haja ya kuwa chonjo kama alivyoeleza Mkurugenzi Mkuu Margaret Chan''Kuna uwezekano kuwa ugonjwa huu utabadilika na ukawa wa hatari:Kwahiyo tunahitaji kuendelea kuwa chonjo ili tuweze kupata maelezo yaliyo sahihi zaidi.''


Sekta ya utalii iliyo moja ya nguzo muhimu ya uchumi ya Mexico inaripotiwa kuathirika kwasababu ya hofu iliyozushwa na homa hiyo.Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha wa Mexico Agustin Carstens athari za ugonjwa huo huenda zikasababisha pato la nchi yake kupungua kwa kiasi cha takriban dola bilioni 70.

Virusi vya H5N1 vinavyotokana na ndegePicha: DPA

Kwa upande mwengine Umoja wa Ulaya umeafikiana kushirikiana katika suala la dawa za kupambana na homa hiyo vilevile chanjo.Tamko hilo limetolewa baada ya Mawaziri wa Afya wa Jumuiya hiyo kukutana Luxembourg hapo jana.Kamishna wa masuala ya Afya katika Umoja wa Ulaya Bibi Androulla Vassilou amesisitizia jambo hilo''Mambo ya msingi ni uratibu wa sawasawa katika Umoja wa Ulaya ushirikiano kati ya washirika wetu kote ulimwenguni,uwazi na kujitolea.Ni lazima serikali ziwe na nia ya kupambana na tatizo hili la afya''


Jumuiya hiyo kadhalika ilipinga pendekezo la Ufaransa la kupiga marufuku safari za ndege zinazoelekea na kutokea Mexico.Kwa mujibu wa Taasisi ya Ulaya ya Kuzuia na Kupambana na Magonjwa ECDC kiasi cha watu 19 wameambukizwa virusi vya H1N1 barani Ulaya.Kisa kimoja pekee cha maambukizi kimeripotiwa katika eneo la Mashariki katika nchi ya Israel.


Vidonge vya TamifluPicha: AP

Katika juhudi za kuziokoa biashara ya nguruwe na bidhaa zake maafisa wa WHO,EU na Marekani wanaendelea kusisitiza kuwa ulaji wa bidhaa hizo kamwe hauongezi uwezekano wa kusambaa kwa virusi vya H1N1.Wanasayansi kwa sasa wamebadili jina la homa hiyo kwa kueleza kuwa virusi hivyo ni aina ya Influenza.Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Misri kuamuru kuchinjwa kwa nguruwe laki nne alfu kama hatua ya kuzuia kusambaa virusi vinavyosababisha homa ya aina yoyote ile.


Marekani kwa upande wake inapanga kununua dosi milioni 13 za ziada za kupambana na homa hiyo zitakazogharimu dola milioni 251.Kwa mujibu wa Idara ya Afya na Huduma za Binadamu za dosi laki nne alfu kati ya hizo zitapelekwa Mexico.

Uingereza imezindua rsami kampeni ya kuwashajiisha raia wake kuosha mikono na kufinika midomo kwa viganja vya mkono kila wanapokohoa au kuchemua ili kuzuia virusi hivyo kusambaa.

Timu za mpira za Mexico Chivas Guadalajara na San Luis de Potos zimeamua kuhamishia mechi zao za kirafiki katika nchi jirani ya Colombia.hata hivyo uamuzi huo unazihussiha mechi za awamu ya pili pekee ya kombe la Copa Libertadores.


Mwandishi: Thelma Mwadzaya/RTRE/DPA/AFPE

Mhariri: Josephat Charo

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW