Muswaada unaohusu marekebisho ya masoko ya fedha wapingwa
27 Aprili 2010Muswaada unaohusu masuala ya kifedha nchini Marekani ambao unaungwa mkono na rais Obama umeshindwa kupita katika baraza la seneti nchini humo hapo jana. Wanachama wa upande wa Republican wameupinga muswaada huo, hatua iliyochangia kuzuia muswaada huo kuanza kujadiliwa.
Katika taarifa yake aliyoitoa baada ya kura hiyo, rais Obama ameelezea kusikitishwa kwake na hatua hiyo.
Muswaada huo unaohusu marekebisho katika masuala fedha nchini Marekani ulitarajiwa kushindwa katika baraza la Seneti, hasa baada ya wanachama wengi wa Republican kujitokeza kuupinga waziwazi, wakiwa na matumaini ya kutafuta makubaliano kamili kabla ya kuanzishwa mjadala juu ya muswaada huo.
Chama cha Demokratic cha rais Barack Obama kimeshindwa kupata kura 60 zilizokuwa zinahitajika ili kufungua njia ya kuanza kujadiliwa kwa muswaada huo, huku wanachama wote wa Republican katika baraza hilo lenye wanachama 100 wakipiga kura ya kuupinga .
Maseneta 57 ndio waliouunga mkono muswaada huo wakati 41 wakiupinga. Rais Obama ametoa taarifa akisema kwamba amevunjwa moyo sana na hatua ya baraza la seneti, ingawa viongozi kadhaa wa chama cha Demokratic wanasema kwamba wana matumaini kwamba pande zote mbili zitafikia makubaliano juu ya muswaada huo wa sheria kuhusu marekebisho katika masoko ya fedha nchini humo.
Rais Obama amesema kukosekana kwa hatua za kuwalinda wateja pamoja na ukosefu wa uwajibikaji wa mabenki makubwa nchini humo katika eneo la Wall street kumehatarisha kuzorota kabisa kwa uchumi wa taifa hilo, na pia kuwasababishia matatizo makubwa mamilioni ya wamarekani, ikiwa ni pamoja na kuwakosesha ajira na makaazi.
Aidha rais Obama ameongeza kusema kwamba muswaada huo wa marekebisho katika masoko ya fedha nchini Marekani, ambao umekuwa ukishughulikiwa na vyama vyote viwili Republican na Demoktratic kwa takriban mwaka mmoja sasa, ndio utakaoweza kuzuia mzozo wa fedha kama ulioshuhudiwa kutotokea tena, hivyo basi amewashauri maseneta wote kushirikiana katika kuangalia maslahi ya taifa kabla ya vyama vyao.
Muswaada huo unataka kuchukuliwe hatua kali za kudhibiti na kuyazuia mabenki kuendesha biashara hatari ya pata potea pamoja na kuwalinda wateja wa mabenki hayo. Wakati huohuo, rais Obama anatazamia hapo kesho kutoa hotuba yake juu ya muswaada huo katika jimbo la Illinois ambako ni kituo cha mwisho cha ziara yake ya siku mbili katika maeneo ya vijijini nchini Marekani yenye lengo la kujadili juhudi za kuimarisha uchumi katika maeneo hayo. Hii leo anatembelea Iowa na Missouri.
Rais Obama pamoja na chama chake cha Demokratic wanataka pachukuliwe hatua kali za kuzuia kujirudia kwa msukosuko wa masoko ya fedha uliotokea mwaka 2008 hadi mwaka2009 ambao ulisababisha mporomoko mkubwa wa kiuchumi. Upande mwingine, chama cha Republican kinaona haja ya kufanyika marekebisho, lakini kinasema muswaada huo wa sheria uliopendekezwa na Wa-demokrats unaegemea mtazamo wa serikali. Miongoni mwa masuala yanayopendekezwa katika muswaada huo wa sheria ni pamoja na kuundwa shirika maalum la kuwalinda wateja, kuzuia taasisi za fedha kufanya biashara ambazo hazimuhusu mteja pamoja na kuweka utaratibu wa kuzivunja benki zinazokabiliwa na matatizo ya kifedha.
Mwandishi Saumu Mwasimba RTRE
Mhariri: Miraji Othman