1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muswaada wa kupinga ushoga kusainiwa Uganda

15 Februari 2014

Rais Yoweri Museveni wa Uganda amesema atasaini muswaada tata unaopinga ushoga na kuwa sheria kamili.

Homosexuelle Demonstration in Uganda
waandamanaji wakipinga muswaada wa kupinga ushoga nchini UgandaPicha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo inaelezwa kuwa ni onyo kwa wanaotetea vitendo vya mahusiano ya jinsia moja kuwa watashughulikiwa vikali nchini humo.

Mwezi uliopita kiongozi huyo alipanga kuachana na muswaada huo ambao umekuwa ukikosolewa vikali na wahisani kutoka mataifa ya Magharibi na wanaharakati wa haki za binaadamu tangu ulipowasilishwa mwaka 2009. Mapenzi ya jinsia moja ni mwiko katika mataifa ya Afrika na kinyume cha sheria kwa mataifa 37.

Wasiwasi wa mashoga wa Afrika

Wanaharakati wa haki za binaadamu wanasema Waafrika wachache waliojitangaza kuwa mashoga, wanahofu ya kufungwa, kukabiliwa na vurugu na kupoteza ajira zao.

Wakati wa mkutano wake na chama tawala nchini Uganda NRM kundi la wanasayasi liliwasilisha utafiti wao kuhusu mapenzi ya jinsia moja kwa rais Museveni. Msemaji wa mkutano huo, wa NRA Anite Evelyn katika taarifa yake alisema kuwa "Museveni alitangaza atasaini muswaada huo kwa vile swali lile la iwapo mtu anaweza kuzaliwa shoga au hapana limejibiwa".

Rais Yoweri Museveni wa UgandaPicha: Imago

Uchunguzi wa mawaziri

Katika taarifa yake kamati ya mawaziri iliyokuwa ikilifanyia uchunguzi suala hilo ilisema Ijumaa (14.02.2014) hakuna vinasaba vya mapenzi ya jinsia moja na kwa hivyo si ugonjwa lakini ni tabia isiyo ya kawaida ambapo mtu anaweza kujifunza tu kwa kupitia uzoefu katika maisha.

Katika mkutano na chama tawala cha NRM, Mshauri wa Rais katika masuala ya Kisayansi, Dokta Richard Tushemereirwe alimwambia kwamba "mapenzi ya jinsia moja yana athari kubwa kwa afya za watu kwa hivyo si jambo la kuachwa liendelee hata kidogo".

Muswaada wa kupinga uhusiano wa jinsia moja uliwasilishwa bungeni mwaka 2009, ambapo awali ulikuwa ukipendekeza adhabu ya kifo kwa wanaoshiriki vitendo vya ngono kwa watu wa jinisia moja, lakini ukafanyiwa marekebisho kwa kuweka adhabu ya vifungo vya awamu gerezani na maisha kwa kile kilichotajwa kuwa mapenzi ya jinsia moja ya kuchochewa.

Rais Museveni alisisitiza kuwa , wahamasishaji, wanaojionesha na wote wanaoshiriki vitendo vya ngono kwa watu wa jinsia moja kwa sababu za ukaidi wa kutumwa , hawatavumiliwa na watakabiliwa vikali.

Mwandishi: Sudi Mnette
Mhariri: Sekione Kitojo

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi