1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Muswada wa kuwapa wabunge waliostaafu malipo ya uzeeni Kenya

4 Agosti 2020

Wabunge waliostaafu nchini Kenya wanaelekea kwenye neema baada ya mpango wa kuwaongezea malipo ya uzeeni kupata kasi mpya.

Kenia Parlament
Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

Hilo litawaongezea wabunge zaidi ya 375 waliostaafu malipo ya uzeeni kutoka shilingi alfu 33 hadi laki moja.mMkenya wa kawaida anayelipa kodi ndiye atakayegharamia nyongeza hiyo.

Wabunge waliohudumu kati ya mwaka 1984 na 2001 wanajiandaa kupokea malipo ya uzeeni ya shilingi laki moja hadi kufa kwao kila mwezi chini ya mabadiliko ya sheria ya bunge ya kustaafu.

Bunge linatarajiwa kuyapigia kura hapo kesho mageuzi hayo yaliyo na azma ya kuwatengea waliostaafu kima maalum cha malipo ya uzeeni wabunge waliohudumu kwa kipindi hicho cha miaka 17.

Kinachobadilika ni kuwaingiza kwenye kundi hilo wabunge waliohudumu kwa muhula mmoja ambao wametengewa malipo ya uzeeni kwa muda fulani na wala sio hadi kufa kwao.

Kitita kwa wabunge wastaafu

Kwa mantiki hiyo, wabunge waliostaafu watapokea kitita hicho cha mamilioni kitakachojumuisha malipo ya kutokea Julai mwaka 2010.

Kulingana na sheria ya bunge ya kustaafu iliyoanza kufanya kazi mwaka 2000,wabunge waliohudumu kwa mihula miwili au zaidi ndio watakaopokea malipo ya uzeeni ya shilingi laki 125 kwa mwezi hadi kufa kwao.

Waliohudumu kwa muhula mmoja watapokea kiwango kilicho sawa na mara tatu ya kile walichochangia kwenye hazina ya uzeeni pamoja na riba ya 15% kwa kila mwaka waliohudumu.

Hata hivyo sheria haikuwajumuisha wabunge waliostaafu kabla ya mwaka 2002.

Familia za wabunge walioaga kupokea malipo yao

Kutokana na hilo, wabunge 290 waliostaafu wataongezewa malipo ya uzeeni yatakayofikia laki moja hai kufa kwao.

Wengine 80 waliokuwa hawamo kwenye mfumo huo watapokea hela zitakazowawezesha kuwa sawa na wenzao waliohudumu kuanzia mwaka 2002. Hao watapokea shilingi laki 125 kwa mwezi.

Ifahamike kuwa wabunge 130 katika kundi hilo tayari wameshafariki dunia kwa hiyo jamaa zao ndio watakaopekea nusu ya malipo hayo kila mwezi.

Mwaka uliopita afisi ya bunge ya bajeti ilibainisha kuwa wabunge hao 290 waliostaafu watapokea kitita cha shilingi milioni 6 kila mmoja.

Waliosalia ambao ni 80 walipangiwa malipo ya shilingi milioni 11.9 kwa mpigo kisha laki moja kwa mwezi hadi kufa kwao.

Endapo mswada huo utapita na kupata ridhaa ya rais, Wakenya wanaolipa kodi watalazimika kugharamia shilingi milioni 180.9 kila mwaka kwa kila mbunge aliyestaafu.

Mwandishi: Thelma Mwadzaya, Nairobi

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW