Rais wa sasa wa Malawi anaongoza katika matokeo ya kura
23 Mei 2019Katika kikao na waandishi wa habari leo, mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Malawi, Jane Ansah alisema katika kura ambazo zilikuwa zimeshahesabiwa, mpinzani wa karibu wa Mutharika, Lazarus Chakwera anafuata kwa kura asilimia 35 na makamu wa rais Saulos Chilima naye yuko na asilimia 18. Ansah ameeleza kwamba kumekuwa na tatizo la uwasilishaji wa matokeo ya kura jambo linalofanya ujumlishaji wa kura kwenda polepole.
"Ningependa pia kuwahimiza raia wa Malawi kuwa makini na matokeo ya kura yasiyokuwa rasmi. Baadhi ya matokeo yanaonyesha namna watu walivyopiga kura na kutoa ishara za matarajio ya nani atakayeshinda ila baadhi ya matokeo hayo sio ya kweli na hivyo yanaweza kusabaisha vurugu, alisema Ansah
Mgombea wa chama cha Malawi Congress yaani MCP, Lazarus Chakwera alisema chama chake kinafanya hesabu ya kibinafsi na hadi sasa yeye ndiye anaongoza katika kura walizozijumuisha, huku akionya wapinzani wake dhidi ya wizi wa kura.
Siku ya Jumanne pia wapigaji kuwa walishiriki uchaguzi wa kuwachagua wabunge. Malawi ina wapigaji kura milioni 6.8 ila tume ya uchaguzi haijasema ni watu wangapi waliweza kupiga kura.
Kulingana na sheria za uchaguzi wa Malawi, mgombea atakayepata kura nyingi ndiye atakayetangazwa kuwa mshindi.
Waangalizi Malawi wasema uchaguzi ulikuwa mzuri
Waangalizi wa kimataifa wametarajiwa kutoa ripoti yao hii leo juu ya namna uchaguzi huo ulivyofanyika ila waangalizi kutoka shirika la nchini Malawi la National Initiative for Civic Education limeshatoa ripoti yake inayoeleza kwamba uchaguzi huo ulifanyika kwa uhuru, usawa na kwa amani. Ripoti hiyo imesema pia kulikuwepo na visa vichache vya mivutano na kutoelewana.
Muadhiri wa maswala ya siasa ya sayansi katika chuo kikuu cha Kikatholiki Malawi, Nandin Patel ameueleza uchaguzi huo kuwa wa mabishano na ushindani mkali.
Malawi ni taifa linalotegemea misaada kutoka jamii ya kimataifa kwa sababu ya viwango vya umasikini ambapo kulingana na shirika la fedha ulimwenguni, IMF, asilimia 70 ya raia yaani kama watu milioni ishirini wanaishi chini ya dola mbili kwa siku.
Rais Mutharika aliingia madarakani mwaka 2014 kwa kupata asilimia 36 ya kura. Uongozi wake ulighubikwa na kashfa kubwa za ufisadi na upendeleo japo mfumko wa maisha uliweza kupungua kutoka asilimia 23 hadi asilimia 11 lakini ni asilimi 11 pekee ya raia wake walio na stima katika majumba yao. .
(AFPE/RTRE)